Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

   Msamaha ni nini, kwa nini tusamehe, nini matokeo ya kutokusamehe? Fuatana nami katika series hii ya fundisho la msingi.

   Mdee Junior, mtumwa wa Yesu Kristo, ndugu yake msomaji wa blog hii, kwa hao walioitwa, waliopendwa katika Mungu Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo, wapate neema ya kusamehe kama vile Kristo Yesu alivyowasamehe. Mwongezewe rehema na amani na upendano ndio tunda la roho ya msamaha. AMINA.

   Msamaha ni: Kufuta deni, kuhurumia, kupatanisha, kuleta / kurudisha mahusiano yaliyovunjika / potea. Ni tendo la upendo, na upendo hauhesabu mabaya.

Msamaha ni kanuni ya MAISHA, Yatupasa kusamehe kwa sababu hatukuitwa ili kubeba hali ya kutokusamehe.

* Iko nguvu inayohuisha ndani ya msamaha ndio maana baada ya kupokea msamaha wa Yesu Kristo unajisikia kuwa mtu mpya / unahuishwa upya.
* Tunapovunja kanuni ya msamaha, tunavunja kanuni ya maisha. Kukataa kuomba msamaha / kusamehe wengine ni KIBURI- maana Mungu alitusamehe.
Samahani ni neno dogo lakini linaweza kusababisha maelfu kuangamia / kuponywa, kanisa kujengwa / kubomoka; laweza kuleta umoja imara / kuvunja umoja, pia laweza kurudisha upendo au kuleta chuki na visasi.
Neno  nimekusamehe linarudisha mahusiano, linaponya na limeponya wengi. Kutokusamehe kunaonyesha uchanga wa kiroho. Pia kunafunua au kuonyesha mahusiano kati ya mtu binafsi na Mungu jinsi yalivyo.
* Kusamehe ni kufuta kila kitu na kuanza upya, na hii inaonyesha mahusiano yaliyo imara na thabiti kati ya mtu binafsi na Mungu na huu ndio UKOMAVU WA KIROHO.

YESU AKASEMA IMEKWISHA.

Yesu kusema imekwisha, maana yake ni kwamba alitusamehe kwa kutuhurumia na ndio maana;
* Tunasimama siku zote kwa sababu ya msamaha wa Bwana Yesu.  Waebrania 12:2b
   'Ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu'...
Watu wengi wameshindwa kuomba msamaha kwa sababu wanahisi wataradhauliwa na kuonekana duni, lakini kumbuka kuwa Yesu hakuwa na mtazamo hasi kama huo ndio maana Biblia inasema kwamba ALIIDHARAU AIBU. Hata kama utadharaulika, ni lazima usamehe maana hii ndio kanuni ya maisha ya Ki-Mungu.
* Yesu ametuachilia na kutuweka huru.

KUTOKUSAMEHE KUMESABABISHA MAJERAHA MENGI - HURTINGS.

Mathayo 18:21-35; Wakolosai 3:14
   Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambii hata mara saba bali hata saba mara sabini.

   Ndugu yangu hapa ndipo kazi ilipo. Kutokusamehe kumesababisha majeraha ya nafsi na uchungu mwingi ndani ya mioyo ya watu wengi. Biblia pia inasema, 'hampati kwa sababu hamuombi' sio kwamba hatuombi kweli bali kwa sababu mioyo imejaa uchungu hivyo hata tuombapo kinachotutoka ni UCHUNGU sio maombi.
   Ili uweze kupona inakubidi ufungue mlango katika moyo wako na kumtoa moyoni yule aliyekuumiza na kukusababishia makovu / maumivu / majeraha; umsamehe na kumwachilia kabisa. Msamaha huleta uponyaji, maisha ya msamaha ni ya kila siku; huwezi kuwa na mahusiano mazuri usiposamehe.
Unapotaka kusamehe usiangalie tatizo linalohusika hata kama wewe ndie una haki bali mtazame Yesu Kristo Msalabani. Yesu hakuwa na hatia yeyote iliyomfanya ateswe na kudharauliwa hata kutemewa mate lakini katikati ya maumivu hayo makali alisema; BABA WASAMEHE kwa maana hawajui walitendalo.

* Mstari wa 21. Hapa Yesu alimaanisha hivi; '' Petro, kumbuka nimekusamehe mara ngapi? hivyo endelea kusamehe sio mara saba tu bali saba mara sabini.
* Biblia inasisitiza juu ya msamaha kwa sababu ndiko kuna UZIMA. Uzima ulitolewa kwa njia ya msamaha - IMEKWISHA.
* Kusamehe sio kujaribu kusahau maumivu / kusukuma hisia chini au kudharau maumivu. Sema kweli / kuwa wazi na mwambie Mungu-Bwana nimeumia.
* Hakuna wakati maalumu wa kusamehe, kusamehe ni wakati wote (24hr) tunawasamehe watu wanapotukosea pia usimwendee mtu huku ukimwonyesha makosa.

   Mstari wa 27. 'Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni'. Kumbe msamaha ni tendo la kuhurumia na lina nguvu ya kipekee katika ulimwengu wa roho maana sisi ni roho.
Usipomsamehe mwenzako, unakuwa umemuweka kifungoni kwenye ulimwengu wa roho na wewe pia maana unajifungia mlango wa kutokusamehewa na kufanikiwa.

   Mstari wa 28-34; Inatuonyesha madhara ya kutokusamehe, kama Mungu kupitia Yesu Kristo aliweza kutusamehe, je! mimi ni nani hata nishindwe kusamehe? Mungu naomba nipe roho ya kusamehe na moyo wa kuachilia.
   Mstari wa 35; Msamaha ni lazima utoke moyoni maana kuna tofauti ya kusamehe na kugandamiza hisia (kubali yaishe).
   Mathayo 6:14-15; Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Matokeo mengine ya kutokusamehe ni kwamba:
1. hutasamehewa
2. Unabeba na kutembea na watu moyoni
3. unakuwa na uchungu juu ya watu waliokuumiza; haya yote yanavunja umoja wa mtu na mtu hata na kwa kanisa pia.
4. unafungua mlango wa wewe kushambuliwa katika nafsi yako na shetani, maana shetani anaifahamu kanuni ya msamaha.
5. Utakuwa unaishi maisha ya mambo / vitu vilivyopita - Isaya 43:18-19. Na matokeo yake ni uchungu-kukandamizwa-roho ya uasi-kupagawa hasira.
Yesu alijua kanuni ya msamaha, naye alikuja ili kutufundisha na kutuingiza katika darasa / shule ya msamaha.

AINA YA MSAMAHA.

1> Kujisamehe wewe mwenyewe; ni ile hali ya kukubali na kuamini kuwa Mungu amekusamehe baada ya kuomba msamaha na kutubu mbele zake. Usikumbuke yaliyopita maana Mungu ana mpango mpya.

2> Samehe wengine; mfano. wazazi wengi wameumiza watoto wao kwa sababu nao waliumizwa. Hivyo samehe wazazi wako, viongozi, jamaa na marafiki zako hata kama wapo mbali nawe.

3> Msamehe Mungu. Kuna wakati Mungu anapofanya kazi yake ndani yako unakuwa unahisi maumivu na kwamba  amekuacha au hakuoni hali ambayo inaweza kukuletea maumivu makali na kumchukia Mungu na kukufanya uwe mtu wa kumlalamikia Mungu kitu ambacho ni kosa. Hivyo msamehe Mungu kwa kumuacha na kumruhusu amalize kazi aliyoianza ndani yako.

4> Samehe tetesi zote. Yale mambo yote yanayosemwa kinyume juu yako, samehe songa mbele huku ukimtazama yeye aliyekuita maana ni mwaminifu hatakuacha.

UNAWEZAJE KUSAMEHE.

a/
Kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hutupa upendo wa kuwapenda adui na neema ya kuwaachilia.

b/ Uwe tayari kusamehe. Peleka moyo wako / hisia zako kwa Mungu naye atakupa neema ya kusamehe. Hisi zako ndio alama (indicator) pekee inayokuonyesha / ashiria kama umesamehe au la!

c/ Jenga uhusiano na adui yako; kula naye, fanya kazi pamoja naye, shirikiana naye.
Msamaha huleta mawasiliano.

HITIMISHO:
UKIJAA UCHUNGU NA MASHUTUMU; UTAKACHOKITOA NI UCHUNGU NA MASHUTUMU.

Mungu wangu na akubariki sana kwa kufuatilia somo hili la msamaha; naamini limekutoa sehemu moja na kukupeleka hatua nyingine mpya katika ukuaji wako wa kiroho na kujenga mahusiano imara kati yako na Mungu na wale wote wanaokuzunguka.
Nimejaribu kukueleza kwa kifupi tu kuhusu msamaha, lakini kama utahitaji ufafanuzi zaidi au kuonana nami ana kwa ana, na kama unahitaji msaada zaidi kuhusiana na kanuni nzima ya msamaha, kama unahitaji maombi; usisite napatikana na nipo tayari kukuhudumia. Wasiliana nami kwa moja ya mawasiliano hapo chini. Pia itakuwa njema kama utaacha comment zako hapo chini. Elezi vile ambavyo Bwana amekufungua kupitia somo hili. AMINA.

Bonyeza hapa kusoma makala zingine za kiuchumi.


MAWASILIANO:

Mobile: +255 653 100 100
Email: mdeejunior@gmail.com
Instagram: wasemeetz

Holding on to the hurt doesn't make it better. If you'll let it go and move forward, God will make it up to you.

GOD BLESS YOU

Mdee F. Junior




«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:


Juu