Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

AL-QAEDA YAHUSISHWA NA SHAMBULIO LA WESTGATE SHOPPING MALL


 
SHAMBULIO la kigaidi lililofanywa nchini Kenya Jumamosi iliyopita na watu waliodhaniwa kuwa wafuasi wa Al- Shabab, sasa limeelezwa kutekelezwa na mtandao mpana zaidi wa kigaidi wa kundi la Al-Qaeda.


Baadhi ya wachambuzi na wachunguzi wa masuala ya kiusalama na kimataifa, wameyataja mambo matatu ambayo yanathibitisha pasipo shaka kwamba waliotekeleza tukio hilo la kuvamia, kuteka nyara na kuua watu wapatao 68 katika Kituo cha Biashara cha Westgate, ni wa aina ya kundi ambalo kinadharia na kimatendo linafanana na lile la kigaidi duniani la Al-Qaeda. Mambo yanayotajwa na wachambuzi na wachunguzi hao ni pamoja na mbinu, teknolojia na aina ya watu waliotumika kutekeleza shambulio hilo.

Katika uchambuzi wao, wameeleza kuwa mbinu iliyotumiwa na magaidi hayo kuvamia pasipo kujulikana mara moja na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchini Kenya, lakini pia aina ya silaha walizokuwa nazo, inaonyesha kuwa kundi hilo limeamua kutumia kivuli cha Al-Shabab kufikisha ujumbe kwa dunia kwamba lipo licha ya uongozi wake kubadilika.

Kwamba mbali na mbinu pamoja na teknolojia, pia aina ya watu waliohusika kutekeleza shambulio hilo ambao wamebainika kutoka katika mataifa mbalimbali duniani, ndio ambao wamewafanya wachambuzi na wachunguzi hao waanze kupata shaka kwamba huenda kuna kundi kubwa zaidi lililotekeleza shambulio hilo, ambalo limejivika taswira ya Al-Shabab.

Watu wanaotajwa kuvamia kituo hicho cha biashara na kutekeleza unyama wa kutisha, wanaelezwa kutoka katika mataifa ya Somalia, Uingereza, Marekani na Syria.

Taarifa hizi zinathibitishwa na kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed ambaye katika mahojiano yake na Kituo cha Televisheni cha Al-Jazeera, alisema kuwa Al-Shabab hawakuwa peke yao katika shambulio hilo.

Mohamed aliiambia Al - Jazeera kuwa al-Qaeda ndio waliokuwa nyuma ya tukio hilo na si Al-Shabab.

“Al-Shabab hawafanyi peke yao, hili shambulio ni sehemu ya kampeni ya ugaidi wa kimataifa,” alisema Mohamed.
Waziri huyo alisema zaidi ya magaidi 20 wakiwemo wanawake, walikuwa nyuma ya shambulio hilo na kwamba watu hao wametoka katika mataifa tofauti tofauti duniani.

“Al-Shabab wanataka kujionyesha kwenye ngazi ya kimataifa, hasa baada ya kubadili uongozi na wanataka kuionyesha dunia kwamba wana nguvu bado, hivyo kuwekwa kwenye kundi la kulifikiria,” alisema.

Katika mahojiano yake mengine na kituo cha cha PBS cha nchini Marekani, Waziri Mohamed alisema washambuliaji kama wawili au watatu wamebainika kuwa ni raia wa Marekani na Mwingereza mmoja.

Ni kutokana na taarifa hizo, baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa shambulio hilo la kigaidi lina ajenda zaidi ya Kenya.
Zipo hisia kwamba shambulio hilo halikuwa na lengo la kuiumiza Kenya pekee, kutokana na hatua yake ya kupeleka majeshi yake kwenda kupambana na kundi la kigaidi la Al-Shabab nchini Somalia, bali pia kumuumiza Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye kwa asili anatoka nchini humo.

Obama ambaye nchi yake imekuwa ikiongoza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ikiwamo lile la Al-Qaeda, ambapo hivi karibuni ilifanikiwa kumuua kiongozi wake, Osama bin Laden, baba yake ni raia wa Kenya.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa, kitendo cha magaidi kuamua kukishambulia kituo hicho cha biashara cha Westgate, kinatokana pia na ukweli kuwa watu wengi wanaopenda kutembelea hapo ni raia kutoka mataifa ya Magharibi wakiwemo Wamarekani, hivyo ulikuwa ni mkakati wa kumuumiza Obama kwa njia hiyo.

Katika hotuba yake aliyoitoa siku ya Jumatatu, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alilielezea kundi la Al-Shabab kuwa ni tishio jipya kwa dunia.



Source: Fahamutz



NAWASHUKURU WASOMAJI WANGU, SASA TUMEFIKIA WASOMAJI ZAIDI YA ELFU ISHIRINI NA NNE 24,000. ENDELEA KUWASHIRIKISHA NA WENGINE.

Juu