Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

SABABU MBOVU ZA KUINGIA KATIKA MAHUSIANO/NDOA.
(Fahamu kwanini wengi hujuta baada ya muda mfupi).



Watu wengi tumewaona kwenye ndoa wakiishi katika hali tofauti za maisha, wako wenye fedha na wasionazo, wako wenye furaha na wasionayo. Yote hii huweza kuchangiwa na sababu nyingi ikiwemo wanandoa hawa kujikuta wanaingia katika ndoa wakisukumwa na sababu zilizo mbovu na zisizo na msingi.

Ziko sababu njema na nzuri za ndoa zinazoongelewa sana na wengi maeneo mbalimbali. Mimi nimejaribu kuzitafuta zile sababu zisizo nzuri ambazo wengine pasipokuwa makini wamezishikilia na kuziruhusu sababu hizi ziwasindikize katika ndoa na hivyo kujikuta wanajuta na kulia katika muda mwingi wa maisha baada ya mahusiano hayo.

Hii pia ni sababu ya ukweli kwamba siku hizi idadi ya ndoa zinazovunjika ni kubwa sana kuliko awali. Hali ya kiwango cha kudhamiria (commitment) kwa wanandoa ni kidogo sana na hivyo kushusha uthamani wa ndoa zenyewe.
Sababu hizi zitakuwezesha kuubadili mtazamo ulionao juu ya ndoa na kukupelekea kubadili namna unavyo sema au kuwaza au kutenda kuhusiana na suala zima la ndoa na mahusiano.

 1. Kuingia katika ndoa/mahusiano kwa lengo la kusaidiwa au kuongeza kiwango cha kiuchumi
     ulicho nacho.

Hapa wengine wamewageuza wapenzi wao kuwa mitaji au rasilimali ya kuwaondoa wao pamoja na ndugu zao kutoka kwenye umasikini. Kwa kuthibitisha hili wengine wamepewa majina kama BUZI, ATM n.k.

Katika penzi la namna hii hakuna mguso au muunganiko wa kuhisia (intimacy) baina ya wapenzi, bali kinachowaunganisha pekee ni kile kilicho mfukoni au vile vinavyoshikika na kuonekana tu. Athari za penzi la aina hii lina fungua milango mingi kwa wahusika kutokuwa waaminifu na hata kujihusisha na mapenzi nje ya mahusiano yao.

 2. Hofu ya umri kupita na kuzeeka.
 
Wako wengi sana, hususani watu wa wajinsia ya kike ambao wamejikuta wakiwakubali wanaume wa aina yoyote ili mradi tu nao waolewe maana umri wao ulionekana kusonga sana na hofu ya kutoolewa kutanda. Mwanaume anayehusiana na mwanamke mwenye tabia hii huulizwa au kulazimishwa kila siku kwenda kujitambulisha kwa wazazi wa binti au kutangaza ndoa. Ndoa nyingi za aina hii zimeishia kenye talaka na kutengana.

Wako wengine ambao kwasababu wanakiu sana ya kupata watoto na wameogopeshwa sana habari kwamba wana weza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, basi watacheka na kaka yeyote yule ilimradi tu waolewe au wazae naye. Wengine wajinsi hii wamejuta sana baada ya kujikuta kuwa waliyezaa naye hakuwa BABA bali mwanaume tu, tena kirukanjia tu na kwahiyo wanawake hawa wameishia kulea mtoto au watoto wao wenyewe pasipo mzazi wa pili (single parenting), jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linawaathiri watoto wengi. Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, kukumbuka kuwa hata huko kwenye ndoa kuna waliokosa watoto.

 3. Kuingia kwenye ndoa sababu ya mimba au mtoto aliyepatikana kabla ya ndoa.
 
Lazima kutofautisha kuwa sababu iliyowapelekea kuzaa mtoto siyo itakayowapelekea kuoana. Acha sababu ya kuoana kwenu iwe penzi lenu la dhati na sio mimba au mtoto. Suala hili linahitaji pia wazazi wajue kwamba kitendo cha watoto kupeana mimba au kupata mtoto hakitoshi kuwa sababu ya kuwalazimisha kuoana, maranyingi wazazi wamewalazimisha watoto wao kuingia katika ndoa sababu ya mimba au mtoto na kujikuta wanawaharibia maisha yao mazima. Yanini kujiingiza katika mahusiano yakudumu kisa umempa au umepewa mimba na kuifanya hiyo ndio sababu ya kulazimisha muishi pamoja kama mume na mke wakati kabla ya mimba hiyo hakuna mmoja kati yenu aliyewahi kuwaza kuwa siku mmoja mtakuwa mume na mke, badala yake baada ya kipindi kifupi mnagundua kuwa hakuna penzi baina yenu bali kinacho waunganisha ni mtoto pekee. Maumivu na vikwazo baina yenu vinawadhihirishia wazi kuwa ninyi wawili hamkutakiwa kuwa pamoja bali mmelazimisha tu. Kinacho fuatia hapo ni kufungulia mlango penzi lingine nje au kufanya mkakati wa kusitisha mahusiano yenu ili kuitafuta furaha ya kweli sehemu nyingine.

 4. Kulazimika kuingia kwenye ndoa au mahusiano ya kudumu kwasababu ya upweke,
     (Loneliness)
 
Mara nyingi mtu anapokuwa peke yake (single) huwaza kuwa ndoa ndiyo inayoweza kuwa utatuzi mkubwa wa matatizo yake. Nakubaliana na ukweli wa maandiko kwamba “Sio vema mtu awe peke yake…” lakini ni vizuri tukijua tofauti iliyopo baina ya kuwa peke yako na upweke. Hivi ni vitu viwili tofauti: kuwa peke yako inamaanisha kukosa mawasiliano au ukaribu na watu wengine, unakuwa kama uliyetengwa (being alone), wakati upweke (loneliness) inahusisha nafsi, akili na hisia (soul, mental and emotions) kuwa pweke au kujihisi kutengwa na hii ni ngumu kuishuhulikia. Ni heri kuwa peke yako (single) kuliko kuwa kwenye ndoa na bado ukajisikia upweke (lonely). Wako wengine waliodhani ndoa ni suluhisho la upweke waliokuwa nao na mara walipoolewa au kuoa, mawasiliano baina yao yakayumba na hivyo kukomaza upweke kwa wote wawili (Not alone but lonely).

 5. Kuolewa au kuoa kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu au marafiki.

Shinikizo hizi zaweza kuwa za kihisia au hata kihalisia. Kihisia ni pale ndugu au wazazi wanapokushawishi mara kwa mara kuoa sababu umri wako unaonekana kwenda na wako wazazi wengine husisitiza kuwa wanataka wajukuu (utasikia mzazi anasema unataka nife sijawaona wajukuu zangu?). Hata kama huhisi kulazimishwa lakini kwa kule kurudia rudia kwa kukumbushwa kila siku kunaweka shinikizo ndani yako, kunaathiri hisia zako na kuweza kukupelekea kuingia katika ndoa isiyopangiliwa. Shinikizo la kimwili au kihalisia ni pale wazazi wanopolazimisha watoto wao kuoa au kuolewa na watu fulani kwa sababu tu ni marafiki zao (family friends) au kwa sababu ya kulinda utajiri na matarajio yoyote binafsi. Ndoa nyingi za aina hii zimekuwa kero na dimbwi la maumivu na machozi, baada ya muda kidogo mna jikuta mali mnazo, wazazi wenu wanapatana na kupendana, lakini nyie kama wapenzi ni maadui wakubwa. Jiulizeni mnaingia kwenye mahusiano kwa furaha yenu au ya wazazi wenu?

 6. Kuamua kuoa au kuolewa ili kupata uhuru.

Hii hutokea sana kwa wale waliozoea kubanwa sana na wazazi katika kila wafanyacho hususani katika maamuzi. Wengine huzikimbia familia zao maana hazieleweki, hazina mpangilio na hivyo kutamani kutoka ili wakaanzishe zakwao wenyewe. Kinadada na kinakaka wanachoka kuamuliwa na kuwekewa masharti ya kuvaa, kula, kufanya mambo, kutoka na kurudi kwa muda kwahiyo wanadhani ndoa ndio itawachomoa kifungoni hapo. Ninaushahidi wakutosha wa baadhi ya ambao walikimbilia katika mahusiano ili kuwa huru na kwa bahati mbaya waliyoyakuta huko kwenye mahusiano yaliwafanya watamani hali waliyoiacha nyumbani kwao ingawa kwa bahati mbaya wakati huo ‘it was too late’.

MATOKEO YA KUINGIA KATIKA NDOA KWA SABABU MBOVU.

Lengo la kuingia kwenye ndoa, liwe zuri au liwe baya ndilo litakalotegemeza aina ya maisha yenu katika ndoa hiyo kuwa ya furaha au ya machungu. Baada tu ya kuoana na huyo mtu wako kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka siyo mingi utaanza kuchoka na kutamani kutoka nje ya hiyo ndoa kwa maana baina yenu hakuna muunganiko wa ndani (emotional attachment) baina ya wanandoa wawili. Na mara nyingi hali hii hupelekea msongo wa mawazo (stress), mfadhaiko wa moyo na kukosa furaha ndani ya ndoa. Na matokeo ya hali hii kumfanya mwanandoa mmoja au wote wawili kuanza kutafuta kutoshelezwa na kuliwazwa nje ya ndoa na hapa vinazaliwa vitu vingine kama uzinzi, kutengana, talaka au magomvi na mifarakano isiyoisha.

KWA NINI NDOA NA MAHUSIANO MENGI HUSHINDWA?
 
Kwa sababu ya kukosa maarifa.
Wanandoa wengi hawajui nini wafanye, nini waelewe ili kufanya ndoa yao zifanikiwe. Thamani ya ndoa na jinsi ndoa inavyochukuliwa sikuhizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu, na hii imewafanya wengine kujikuta wako wenye ndoa kwasababu mbovu na hivyo ndoa nyingi kuvunjika au kuyumba baada ya muda mfupi tu. Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu sio vya maana tena siku hizi, sababu watu wanaogopa kuonekana wazamani na washamba.

Mtazamo wa ulimengu juu ya ndoa umeharibiwa na magazeti, luninga na vitabu mbali mbali. Siku hizi kuishi bila ndoa ni kitu cha kawaida, kuwa na mpenzi nje ya ndoa sio kitu cha ajabu tena, mapenzi nje ya ndoa sio ya kushangaza hata kidogo. Kinyume chake ukionekana kuyashangaa haya, jamii itakushangaa wewe kwa jinsi ulivyo nyuma ya wakati. Mambo yamebadilika sana, zamani binti akikutwa bikira wakati anaolewa ilikuwa sifa kwake na familia nzima, siku hizi binti akikutwa bikira atachekwa, na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani. Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya sana tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa kweli na kudhamiria katika mahusiano. Jamii isiyoamini katika uaminifu, na ndiyo maana magomvi mengi hutokea pale simu ya mmoja inapoguswa. Kuwindana na kuchunguzana kumekuwa kawaida, maadili sio jambo la kuzingatiwa tena. Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya moyoni na walio umizwa, kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao wakitafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili waliwazane.
 

SEHEMU YA MWISHO:

Kwa haraka tuangalie sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie katika ndoa na usijute.
- Ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja
- Ni nafasi ya wawili hawa kuonyeshana mapenzi yao
- Ni nafasi ya kutimiziana mahitaji ya mwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi, na kwa mtu sahihi, maadili
  yakizingatiwa.
- Hamu na kiu ya kutengeneza familia yenu.
- Kutimiza kiu ya kuwa pamoja kwa umoja (companionship)
- Nia au kusudi la kushiriki vyote kwa pamoja . Kufanya kutenda kwa pamoja ili kutimiza mahitaji yetu
  wote
- Nafasi ya kutumia kwa manufaa kila uwezo na vipawa mlivyokuwa navyo.
- Kuchangiana katika makuzi yenu ya ujumla, makuzi ya kimwili, kiriho, kihisia n.k

MWISHO:

SOMO LINALOFUATIA

"MAMBO 7 AMBAYO MARA CHACHE SANA UTAAMBIWA AU KUYASIKIA KUHUSU MAHUSIANO/NDOA"
 

KUMBUKA: 
Kama ambavyo Blog hii imekuwa ikikuletea mafundisho yenye kubadilisha ufahamu/akili na maisha kwa ujumla; Unaweza kui-support Blog hii kwa kununua mafuta halisi ya alizeti yenyo ubora wa juu, Lengo ni kufanikisha Blog hii Iendelee kukuletea mafundisho mazuri kutoka kwa watu maarufu na waliofanikiwa ambao nimekuwa nao bega kwa bega ili kuhakikisha msomaji wangu anapata kitu kitakachoweza kumtoa hatua moja kwenda hatua nyingine!
   Ili kujipatia Mafuta haya waweza kuwasiliana nasi kwa  0659 700 002 na Mungu atakubariki.
Asanteni sana wadau wangu! 



 


«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:


Juu