Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

KUNA WATU WANAOKUJA DUNIANI KIMYA KIMYA NA KUONDOKA KIMYA KIMYA

Harris Kapiga_The Critical Thinker.
Msikilize hapa, akiwa ndani ya Nchi Ya Ahadi, Sinza!

WAOGA HUFA MARADUFU KABLA YA KIFO HALISI.

By. Paul Mashauri.

Daima fikra ya mali isiyo kadiri ni mzigo usiochukulika ndivyo LIFE CHANGERS MEDIA chini ya mtumishi wa Mungu, Mwinjilisti, Mwalimu na Mjasiriamali MDEE JUNIOR [ bofya hapa ku-Like Page
ya ujasiriamali ], naamini kuwa mafanikio huanza kwa fikra ya mtu kupata chakula bora cha ubongo, kwani moyo wa mtu hulogwa na upendo ila fikra komavu ziletazo uzalendo na mabadiliko hutokana na elimu ifaayo.
Hii ni kwa sababu maarifa yafaayo huja kwa elimu ifaayo. Hivyo Blog hii inaendelea kuwaletea elimu sana wasomaji wake wote ambao wanahitaji kupiga hatua Kiuchumi kwa kuwapa maarifa toka kwa Watanzania wachache wazalendo wenye utayari kutoa maarifa ya namna ya kufanikiwa katika mipango waliyo nayo ya kimaisha. Hakika elimu hii itakutoa katika ulimbo ambao ulikuwa umekunasa mithili ya kundi la ndege lisilojua ulimbo ulipo.
''Waoga hufa maradufu kabla ya kifo halisi''   Mshirikishe mwenzako juu ya blog hii/share to your friends about this Blog.

USHUHUDA MFUPI WA MAISHA YA ''PAUL MASHAURI''

Hunenwa kuwa ''Watu huogopa; tena huwa na hofu juu ya mambo ya kesho''. Lazima tuelewe hofu tumeumbwa nayo. Binadamu kama wanyama wengine ana hofu. Tambua kuwa hofu ni kitu cha kawaida. Katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi hofu mioyoni mwa watu wengi ni kuhusu maisha. Yaani kutoka sehemu moja ya maisha kwenda sehemu nzuri ya kimaisha.

Hata mimi (Paul Mashauri) niliwahi kuwa na hofu ya maisha hasa baada ya baba yangu kipenzi kufariki nikiwa bado mwanafunzi wa elimu ya chini kabisa. Nakumbuka baba alipofariki tu maisha yalibadilika na kuwa magumu. Nilikata tamaa kuhusu kuendelea kimasomo. Nilijiuliza maswali mengi endapo ningeweza kuendelea na masomo ya ngazi nyingine. Lakini baadae nilifanikiwa kufika chuo kikuu. Nikiwa chuo kikuu hofu haikuniisha kwani nilihofu kuhusu mustakabali wa maisha yangu, mama yangu, na ndugu zangu. Nakumbuka siku moja nikiwa chuoni mimi na rafiki yangu tuliishiwa fedha za matumizi nilitoka chumbani na kumfuata rafiki yangu aliyekuwa ameketi nje na nilimvamia kwa swali:

''Kwanini tunakufa njaa wakati sisi ni wasomi? huku macho yetu yakitazamana''. Tuliingia ndani ambako tulikaa chini na kutafuta kalamu na karatasi na kuandaa mpango mkakati wa kuanzisha gazeti. Hata baada ya kumaliza chuo na kuanza mchakato wa kutafuta ajira hofu bado zilitutawala mimi na marafiki zangu. 
Kwa mara ya kwanza tuliamua kuanzisha jarida letu kwani ndoto ya kuwa na gazeti letu iliota na kusambaa mwilini mwetu. Kazi hii haikuwa rahisi kwani tulipitia katika changamoto nyingi za kukosa hata pa kulala lakini tulishindwa. Wenzangu wakaamua kwenda kutafuta kazi na wakafanikiwa. Baada ya siku kuisha tulianzisha tena gazeti ambalo tuliliita familia. Waandishi wa gazeti hili tulikuwa sisi wenyewe na marafiki zetu ambao walituandikia bure makala ambazo zilizokuwa zikipatikana katika gazeti letu. Hapa napo pia tulishindwa. 

Awamu hii hali yangu ilikuwa ngumu zaidi mpaka niliamua kumrudisha mke wangu nyumbani kwao kwanza na akaanza kupika na kuuza vitumbua, mimi nilikuwa nimebaki mjini malazi yangu yalikuwa ofisini. Wakati haya yote yakinikumba hofu kuhusu maisha haikuniachilia. Ninachokumbuka katika changamoto nyingi nilizokuwa ninazipitia ndani yangu kulikuwa na maono. Niliamini daima kuwa wakati wangu upo... unakuja! Hadi leo nasimama mbele yenu Watanzania wenzangu niliweza kukabiliana na hofu. 

Naomba turejee katika swali letu la msingi linalozungumza kuwa unawezaje kuondokana na hofu. Hatua zifuatazo zitakusaidia nama ya kuondokana na hofu: 

NAMNA YA KUSHINDA HOFU.

1] Kuwa mwenye maono makubwa.

Maono ni namna unataka kuwa maishani. Unapokuwa mwenye maono moyoni au nafsini mwako hutababaishwa wala kukatishwa tamaa na yazungumzwayo na watu juu yako. Tambua kuwa mawazo yako ni makubwa kuliko nyumba. Siku moja baada ya anguko la pili la gazeti gari langu nililiuza hivyo nikaanza kupanda daladala nilikutana na dada fulani ambaye aliponiona alinikaribisha katika daladala kwa kauli ya mshangao:

'Mashauri!...mimi nami nilimjibu.
''Mimi ndiye!!!..

Daima ukiota njozi kubwa hutakatishwa tamaa wala kuona aibu. Kumbuka kuwa kiongozi au tajiri huandaliwa. Panga mambo yako tena usiogope kuwa utafikaje huko au utavipataje, jua tu kuwa utavipata tu. Hivyo, mtu mwenye maono makubwa huondokana na hofu kwani anajua kuwa mapito ayapitiayo ni ya kitambo tu, au ni daraja tu. 

2] Ambatana na marafiki ambao wana mtazamo chanya.

Hebu ifanyie nafsi yako udodosi juu ya marafiki unaoambatana nao. Jiulize nini mchango wao tangu umekuwa nao kama marafiki zako. 
Tambua kuwa ili uweze kufanikiwa katika maono yako lazima 
> Uambatane na watu wenye ndoto. Watu ambao wakati wote wana mawazo chanya, wasiokata tamaa.
> Usikae wala kuambatana na watu ambao kila kitu kwao ni hasi tu.
> Tafuta watu ambao watakutia moyo, watu ambao utajifunza hatua zao za mafanikio mpaka hapo walipofikia.
> Jiwekee mpango wa kukutana na watu wapya kila siku wenye tija.
> Epuka marafiki wakujazao hofu katika mipango yako. 

Kumbuka kuwa biashara ni urafiki tena ulio katika mpangilio uliotukuka. Mfano mzuri ni kwetu (Paul Mashauri) wakati tulipoanzisha gazeti la Familia marafiki zetu wengine ndio walikuwa waandishi wa makala mbalimbali katika jarida hilo tena walifanya bure hawakudai malipo hata siku moja. 
Daima yakupasa kukumbuka kuwa ''Rafiki aliye karibu ni zaidi ya ndugu wa mbali''. Kuwa makini na aina ya marafiki ulio nao.

3] Orodhesha hofu zako.

Chukua karatasi na kalamu orodhesha hofu zako. Baada ya kuziorodhesha chukua muda kuzitafiti ili uweze kujua kiini na namna utakavyoanza kuzikabili hofu zako. Chukua hatua ya kuzungumza na watu unaowaamini kuwa wanaweza kukusaidia kuondokana na hofu zako. 

Mfano: Watu wengi huogopa kuanzisha biashara fulani kwa kudhani kuwa lazima uwe na mtaji mkubwa lakini ukianza kuchambua unaweza kukuta watu hukopa huku na kununua bidhaa na kuuza kisha baadae kulipa deni. Hivyo, njia pekee ya kukabiliana na hofu ni kuikabili hofu yenyewe. Utakuta mtu mwingine anaogopa kusimama mbele ya kadamnasi kuzungumza, tambua kuwa dawa pekee ni kuzungumza.

Kuna athari za hofu ambazo ni kuanguka, kupata mshtuko, pengine mtu hufa. Hivyo ukishazifahamu hofu zako anza kukabiliana nazo. Sisi baada ya biashara ya gazeti kufa  hatukukata tamaa, tulianzisha kampuni nyingine ambayo inajulikana kwa jina la East Africa Speakers Bureau yaani kwa kifupi ( EASB ) kampuni yenye malengo ya kuwasaidia watu waweze kufikia ndoto zao. Wakati tunaianzisha hatukuwa na fedha isipokuwa tulikuwa  na moyo wa kujali.

4] Usiogope kushindwa.

Ipo siri kubwa katika kushindwa. Duniani watu walioshindwa sana ndio waliofanikiwa. Tambua kuwa kushindwa jambo ni kuandaliwa si kwamba una mkosi. Inakupasa kuelewa kuwa kushindwa hakuishi katika maisha ya mwanadamu hii ni kwa sababu tunatakiwa kujifunza kila iitwapo leo. 
Kuanguka kwa gazeti letu nilijifunza, kwani ilinipa changamoto za kujua kwa nini lilishindwa, na hapo tulipo kwenye kampuni yetu mpya ya EASB ni kwa sababu kale tulishindwa.

> Daima kutenda makosa ni fursa ya kuanza tena, pia ni nguzo itakayokuinua tena. Ipo kauli isemayo kuwa 'Maisha ni nyumba' daima ukitaka kuingia ndani lazima upitie mlango mmoja kisha milango mingine.
> Mkwamo hukusaidia kujipanga. Sisi tulijipanga na kuchukua changamoto kama ngazi za kupandia hapa tulipo. Hivyo kutokuogopa kushindwa huondoa hofu ya kutokufanikiwa.

5] Elewa nini maana ya mafanikio.

Kabla ya kuanza kuyasaka mafanikio lazima uelewe dhana ya mafanikio kuwa ni nini? Maana wapo wanaodhani mafanikio ni kuwa  na majumba, magari, fedha nyingi bila ya kujua/kufahamu kuwa hata ukiwa na hivyo vyote kama una msongo wa mawazo, hofu, huna amani nyumbani, huwezi kujiepusha na hofu. Utaona hayo unayoyaita mafanikio si kitu wala si chochote. Ndio maana dunia ya leo hatushangazwi na habari za matajiri kujinyonga, kunywa sumu na kutoweka duniani. 

Ili uweze kuwa na mafanikio yenye furaha huna budi yapitie katika vichokoo vifuatavyo:

Kiroho (spiritual). Mafanikio ya kweli daima huanza na kutengenezwa moyoni. Moyo wako ukiwa na amani, ndugu, jamaa na marafiki wakiwa na amani basi hofu haitamea mtimani mwako.

Utatengenezaje moyo wa furaha:
   * Kuwa mkweli daima.
   * Jali wengine
   * Mshike Mungu, kwani hakuna mtu wala kitu kishindacho imani.
   * Tembea katika maadili.

6] Panua maarifa yako. 

Kama ilivyo kwa afya njema chakula ni muhimu ndivyo ubongo nao unavyohitaji kupata chakula chake ili kuufufua na kuuweka  katika ufaafu wa habari.
Jijengee tabia ya kusoma vitabu, magazeti pia jifunze kutoka kwa wengine. Ongeza maarifa kupitia vyanzo mbalimbali vya maarifa.

Daima tambua kuwa mwili wenye kichwa kisichokuwa na maarifa hata chembe ni mzoga unaostahili kuliwa na fisi au tai.
Sikiliza mazungumzo ya watu wengine. 

   Mfano ni mimimwenyewe nilitamani kuwa kama Erick Shigongo tangu nikiwa darasa la sita ndoto hiyo nilikuwa nayo hadi sasa amekuwa rafiki yangu na Dr. Reginald Mengi huwa nawasikiliza na kujifunza toka kwao. Na ili kuweza kuulisha ubongo wangu na kuuchavusha kila mwezi nimejiwekea ratiba ya kujinunulia kitabu kimoja. ''Kumbuka kuwa maana japo ya wino hafifu ni bora kuliko kauli nzito''

7] Kuwa mwenye afya njema (physical fit).

Tambua kuwa mwili wako unaweza kukufanya usifikie mafanikio yako, inasemekana kuwa magonjwa ya mwanadamu chanzo chake ni mfumo wa maisha yake. Hivyo ukiujali na kuutengeneza vyema mwili wako kwa uangalifu utaondoa hofu ya kifo, hofu ya kutokufikia malengo yako. Jali maisha yako.

8] Kuwa mwenye tabia njema (social wellbeing).

Je, nikija mtaani kwenu nitasikia watu wanasema nini juu yako. Tambua kuwa watu ni mtaji. Unapokuwa na watu jaribu kuwa msikilizaji tu.
Wape nafasi wakueleze vya kwao ya kwako yawe ya mwisho. Usiwe mbishi. Tengeneza mahusiano ili uweze kuwa na sifa njema ambazo hata mtoto wako zinaweza kumbeba hapo baadae.

Namna ya kutengeneza mahusiano yenye tija katika jamii yako.
* Shirika katika shughuli mbalimbali kama vile harusi, misiba n.k
* Usiwe mbishi
* Shiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiutamaduni kwani mtu hujitengeneza anavyotaka kuwa.
* Hakikisha uwezo ulio nao unajulikana kwa watu
* Ondoa uoga
* Fanya vitu vyako vionekane
* Tambua kuwa imani na kumtanguliza Mungu katika kila ulifanyalo, kwani imani inakusaidia kukabiliana na hofu
* Amini kuwa umeumbwa kwa makusudi maalum. Jiulize wewe mwenyewe kuwa upatapo changamoto huwa unamtumaini nani?

CHANZO / ASILI YA HOFU

Hofu huweza kutokana na:

/ Picha zilizojengwa akilini mwetu.
Hii husababishwa na mazingira ambayo mtu husika amekulia au anayoyaishi ama aliyoyaishi. 
Mfano, mtoto mdogo wa kike anaweza kubakwa na mwanamme hivyo kila atakapokuwa  anamuona mwanamme atakumbuka tukio hilo.

/ Kupandikizwa na watu wengine.
Hii inatokana na maneno tunayonenewa na ndugu, jamaa na marafiki zetu pindi tuamuapo kufanya jambo fulani hususan mambo yajayo kinyume... kauli kama hizi ''tulijua tu hautaweza''

/ Taasisi za kijamii. ( familia, elimu, mfumo wa nchi )
Mazingira ya nyumbani huweza kusababisha hofu katika maisha yetu.
mfano, taasisi ya ndoa kila leo unakuta vurugu tu baba au mama huweza kupanda mbegu ya uoga kwa watoto. Pia kutoandaliwa vyema kielimu husababisha hofu.

/ Mfumo wa nchi ( mfumo wa kiuchumi ).
Tulifuata misingi ya ujamaa katika uchumi wetu kwa kufanya kazi kwa pamoja, hakuna aliyefanya kazi pekee lakini sasa tupo katika mfumo wa kibepari unaoruhusu mtu mmoja kumiliki njia kuu za uzalishaji mali na kumudu shughuli zote. Hivyo, mfumo wa uchumi unapobadilika huweza kuzua hofu.

/ Uongozi.
Ukiwa na kiongozi muoga basi watu wake wanaomfuata watakuwa waoga.Hivyo, kiongozi lazima awatoe watu wake hofu na woga.

Tambua kuwa:
 * Kuanza si kupitia mahali pazuri, lazima upitie changamoto
 * Usijihisi mnyonge kwa sababu dunia ya sasa haiwataki wanyonge.
 * Anza wewe mwenyewe
 * Usikurupuke katika kutenda au kuamua.
 * Penda kufanya kitu ukipendacho.
 * Tambua kuwa hata unapojihisi umefanikiwa usisahau mambo yaliyokufanya ufike hapo hasa changamoto
 * Wakati mwingine mafanikio hayaonekani.

WOGA.
Asili yako ni nini
Chanzo chako ni nini
Dawa yako ni ipi
         AU
Dawa yako ni yowe
Dawa yako ni woga?
Dawa yako ni umati?
 Hakika... waoga hufa maradufu kabla ya kifo halisi..

Comment kama imekusaidia kwa namna moja au nyingine: 
contact: 0659 700 002

 


Juu