Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

UMASIKINI UMEMTAMBULISHA SANA YATIMA KULIKO UYATIMA WENYEWE.

Hezekia Mwalugaja - Mkurugenzi na m'beba maono wa Kituo cha Hananasif Orphanage Azungumza na Blog Hii.

Mara nyingi unamtambua yatima kwa sababu anavaa vibaya, hali vizuri. Lakini yatima sio lazima avae vibaya au ale vibaya na hiyo sio tafsiri ya Yatima.
Tafsiri ya yatima ni kuondokewa wazazi lakini pia sio kufiwa wazazi. 
Tuna watu katika ulimwengu tunaoishi wana jina la kuitwa yatima japo hawajapoteza wazazi (hawajafiwa).

Kwa hiyo kigezo kikubwa ni mazingira yanayomzunguka ndo utambulisho wa kwanza wa mwenye sifa  ya kujiunga na shule hii ya HOCET ama kituoni Kinondoni. Hivyo anaweza kuwa amefiwa na wazazi au hakufiwa lakini ana maisha mabaya kuliko wanaoitwa wamefiwa na wazazi.


Ikiwa limebaki Juma moja kabla ya Lile Tamasha kubwa la kumsifu Mungu pamoja na Watoto wa Mungu kutoka kituo cha watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu kijulikanacho kama HANANASIF ORPHANAGE CENTER (HOCET), Blog hii leo tarehe 15-06-2013 Imetembelea kituoni hapo ''Mkuranga Base'' ( HOCET SECONDARY SCHOOL ).
LENGO LA TAMASHA HILI NI KUCHANGIA KITUO HIKI CHA WATOTO YATIMA_HOCET 
 
Jambo la kwanza ambalo liliifanya blog hii istaajabu ni pale Mkurugenzi alipoonyesha jengo lenye vyumba vitatu vya madarasa ambalo lilijengwa kwa siku sita (usiku na mchana), I was like woooow!

Shule hii ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 40 na walimu wa 3, Lakini kwa sasa ina wanafunzi 100 na walimu 8. Shule hii inachukua wanafunzi wa imani zote. Watoto hawa wanapatikana kutoka nchi nzima kupitia Serikali (ustawi wa jamii) na makanisani ambako kuna huduma za ustawi wa jamii.

Mkurugenzi, Hezekia Mwalugaja aliendelea kwa kuelezea lengo la mfumo wa maisha hapo kituoni.
Namnukuu: '' Lengo la kubadili mifumo ya kuishi ni kwa sababu maisha ya watu ambao tunaishi nao ni yale ambayo yametoka kwenye maisha magumu. Hivyo ili kuwaondoa kwenye maisha magumu ni kuwajengea uwezo wa kubadilisha mazingira(environment) waliyozoea ili waishi kwenye maisha mengine ambayo yana matumaini ambayo yanajumuisha elimu (formal & informal education) na kuinua vipaji/vipawa vyao ili wasiishie kutegemea tu akili ya kufundishwa bali pia ya kuzaliwa nayo (TALENT)''.

Maelezo yafuatayo yalitokana na maswali kutoka kwa Blog hii na waandishi mbalimbali wa habari ( Tv na Magazeti ) kama vile Clouds Tv, Tbc, Wapo Radio, Gazeti la Nyakati, Tanzania Daima na Jibu la maisha ambao nao walikuwepo eneo la tukio.

Kituo cha HOCET-Mkuranga kina jumla ya watoto mia moja na kumi (110). Watoto 100 wanasoma hapo na wengine 10 wanahudumiwa kwenye kituo cha mjini (Kinondoni). Hadi sasa kituo kimeshatoa kidato cha nne mara tatu.

Historia fupi ya HOCET.
Kituo kilianza mnamo mwezi Disemba 2002 pale Hananasifu Kinondoni kipindi cha kuelekea Christmas kwa sababu hiyo ndipo likazaliwa wazo kwamba:
Kristo haji kwao waliokuwa na unafuu wa maisha  bali kwao ambao hawamjui na hawana unafuu wa maisha ili nao ujio wa Kristo uwe sehemu yao.

Mungu hakutupa  kutunza yatima kwa wakati huo bali kuzungumza na kanisa kuhusu kujali na kutunza yatima kwa sababu kanisa limeondoka kwenye wajibu na kuachia jukumu lake kwa NGO's. Lakini kabla ya kuliambia kanisa/mtu mwingine ilibidi sisi wenyewe tujifunze kwanza namna iliyo bora ya watoto yatima ili tuwe tumevaa viatu (kubeba jukumu) kabla ya kuhamasisha wengine.
Aliendelea kusema, tunawafundisha watoto kuishi maisha ya kiroho na kumtumaini  Mungu ili watambue kuwa kuondokewa na wazazi wao sio sababu ya wao kuwa na maisha mabovu/magumu.

Aidha, alienda mbali zaidi na kusema; tumekusudia kuwapa elimu ambayo italeta majibu katika maisha yao. Pia lengo la kuwaweka katika shule ya bweni ni ili kwamba baada ya vipindi vya masomo ya kila siku darasani wasirudi mtaani (USWAZI).

Vyanzo vya mapato.
Alipoulizwa, Mwalugaja alisema;
Kituo cha HOCET kina vyanzo vikuu viwili vya mapato ambavyo ni:
i> Networking.
Huu ni muunganiko/mwitikio wa waumini wa imani ya Kikristo na wale wa imani nyingine isiyo ya Kikristo kwa maana ya Watanzania wenye nia moja, dhamiri moja na moyo mmoja kwa kuleta sadaka zao.

ii> Vipawa vya watoto (TALENT).
Tumeinua vipawa vya watoto kwenye eneo la uimbaji. Watoto walifanikiwa kurekodi albamu yao ya kwanza inayojulikana kwa jina la NAJA KWAKO ambapo kazi hii iliuzwa mnamo mwaka 2006 na kuingia mapato kwa ujumla wake zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni ishirini ( 20Ml).
Pia uuzwaji wa albamu hii uliendelea kutengeneza network kwa watu wa ndani ya kanisa na nje ya kanisa kupitia ujumbe uliomo kwenye albamu hiyo.

Blog ilitaka kujua kuwa Mkurugenzi Mwalugaja alitaka nisikie nini na Watanzania wajue nini na wafanye nini kwa ajili ya kituo hiki. 

Ndipo alipofunguka zaidi na kusema:
Watanzania tunalo tatizo la kufikiri kwamba hatuwezi. Tunataka.
Tunataka kujenga uwezo wa Watanzania mkiwemo ninyi (waandishi) kwamba tunaweza pasipo mtu wa pili (mfadhili kutoka nje).
Ili tusonge kama taifa ni lazima tujiamini kuwa tunaweza ili wanapotokea watu kutoka nje ya nchi au nje ya familia yako kukutegemeza (support), wawe wanakutegemeza kwa sababu kuna kazi unayoifanya sio wao wawe sababu ya wewe kuwa na kazi unayoifanya. (hakika niliipenda hii point).
Tunataka Mtanzania wa leo afahamu kwamba mambo anayoyafanya anaweza kufanya mwenyewe. Unajua hawa watoto huko mtaani wamefanywa kuwa hawawezi kitu, lakini sisi kama huduma tunasema wanaweza kitu.

Ni lazima tuwajengee mfumo wa kufikiri zaidi kwamba wanaweza kuliko walivyofikiri kwamba hawawezi. Na ili haya yote yaweze kufanikiwa yanahitaji vitendea kazi, umoja wa dhati na sio umoja wa kuzungumza tu. Aliongeza kusema kuwa gharama za kuendesha shule kwa mwezi ni takribani milioni 15 kwa mahitaji ya msingi.

Mtazamo wa kituo juu ya kuchangisha fedha (fund raising)
Sisi kama kituo hatuamini katika kuchangisha fedha sana kila mahali bali tunafanya kazi sana itakayoleta fedha sana kwa ajili ya kuendesha maono.
Hivyo basi, ombi la msingi kwa Watanzania ni ''KUUNGANISHA NGUVU'' kama Watanzani tuweze kujivunia vitu vyetu hatimaye tuseme hivi ni vitu vyetu, hii ni akili ya kitanzania / kiafrika na sio wageni.
Kwa hiyo msaada tunaohitaji kwa media na watu mbalimbali  TUUNGANE PAMOJA kwamba tunaweza bila kujali ukubwa wa gharama. Tuseme tunaweza katika yeye atutiaye nguvu, hii itatusaidia kuwaonyesha watoto uhalisi wa maisha kwa vitendo.

Blog iliendelea kudodosa ni kazi zipi kituo kinafanya mbali na zilizotajwa hapo awali kuleta fedha za uendeshaji wa kituo.
Mwalugaja akaeleza;
Kituo kina eneo la kutosha kufanya miradi mbalimbali.
Hadi sasa kituo kina ng'ombe kumi wa maziwa lakini lengo ni kuwa na ng'ombe 25 na kusudi ni kuwafundisha watoto kuweza kuona fursa nyingi kutoka kwenye ng'ombe maana ni zaidi ya kupata maziwa na samadi. Pia kituo kina mradi wa kuku wa kienyeji ambapo tayari wameshanunua mashine kutoka China yenye thamani ya Dollar za Kimarekani 2000 ambayo tayari ipo kituoni na pia wameshaagiza mayai kutoka Malawi na Morogoro nayo tayari yapo kituoni na kazi ya kutotoa vifaranga imeshaanza.

Blog hii ilimalizia mahojiano na MkurugenzI, Mwalugaja kwa kutaka kujua nini changamoto kama kituo kwa ujumla wake.

changamoto: NAMNUKUU.
* Namna gani Watanzania wanaweza kukubali kubaki kwenye mambo tunayoweza sisi wenyewe zaidi ya kusema ni lazima wafadhili wapatikane, na hapo ndipo shida inapotokea kwa sababu wafadhili wao ndo wanataka watupe mashari lakini sio sisi tuwape masharti ya kile tunachokifanya na hii ndio changamoto kubwa ya ujumla.

Lakini kwa upande wa elimu; Idadi ya walimu tulio nao hailingani na vile tunavyohitaji kwa sababu hatuna bajeti inayokidhi kuongeza walimu. Sababu nyingine ni namna ya kupata chakula cha kutosha kulisha shule nzima ikizingatiwa kuwa hakuna mtoto hana mmoja anayelipa ada.
Miundo mbinu haijakamilika, huduma za afya ziko mbali sana na kituo hivyo kuna changamoto ya usafiri pia.
Changamoto nyingine ya msingi ni kwamba, Jamii iliyowaombea watoto nafasi ndio yenye huruma na watoto kusoma, lakini watoto wenyewe hawana bidiii ya kusoma kama tulivyotarajia na ile ambayo walezi waliitarajia. Tunajaribu kuikabili changamoto kwa kuwafanyia watoto ushauri na saikolojia kwa msaada wa walimu kutoka Chuo Kikuu cha DSM.

Blog ilihitimishia hapo, na zifuatazo ni baadhi ya picha katika tukio.
Ukitaka kuwasiliana nasi kwa tukio lolote, tupigie kwa namba hii:
+255 659 700 002. 


Mwalugaja akionyesha ramani ya jengo la shule

mkuu wa shule ya HOCET

wanafunzi


sehemu ya madarasa


MC Lawrence Mwantimwa

Bloggers

Noel Tenga

Joshua Kisaka katikati

Waandishi wa habari

Joshua Makondeko

staff room



Sam Sasali Papaa

wanafunzi wakijiandaa na mtihani wa hesabu.

Blogger Mdee Junior akidadisi kitu kutoka kwa wanafunzi hawa.



 Long Live HOCET.






Juu