Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

Ni mara chache sana kwa watu waliofanikiwa kutoa siri za kufanikiwa kwao hasa sisi wabongo. Ni kwa sababu hatupendi kuona wengine wakifanikiwa kwa hofu kuwa wanaweza kutupita katika mafanikio na kuwa juu zaidi yetu!

Lakini haikuwa hivyo kwa Erick Shigongo (A Success Coach) kama anavyojiita. Akiwa ndani ya Nchi Ya Ahadi, semina ambayo ilihudhuriwa na watu wasiopungua 150 alitoboa siri ya mafanikio kwa anayetamani kufanikiwa. Alieleza kanuni rahisi sana za jinsi gani mtu anaweza kufanikiwa, ni kanuni rahisi lakini zenye kuhitaji NIDHAMU ya juu.

                                                                Erick Shigongo alianza hivi:

Kuzaliwa na kuishi duniani ni kutimiza kusudi la Mungu. Lipo kusudi ambalo Mungu analitaka ulitimize katika dunia hii nzuri yenye vitu vizuri vilivyoumbwa na Mungu. Hivyo ipo sababu ambayo ipo mbele za Mungu aliyokupa wewe uzaliwe mahali ulipo.

Wengi wetu tumezaliwa tukiwa na vipaji vingi na wenye uwezo mkubwa lakini wapo walioondoka katika ulimwengu huu bila ya wao kufahamu uwezo uliopo ndani yao. Kutokana na hali ya kutojitambua imewafanya kuhakiki ule usemi usemao kuwa:

'' Makaburini ndiko mahali walipolala watu wenye utajiri mkubwa ''. Utaji ambao walipokuwa hai hawakuujua wala kuutambua uwezo wao ambao kama wangeutambua basi leo hii ulimwengu ungekuwa ukishuhudia maajabu chanya kwa waliyoyafanya. Hivyo basi, kuondoka duniani bila kutimiza kusudi na wajibu wako kwa jamii yako ni kitu kibaya mno.

VITU MUHIMU VYA KUZINGATIA KWENDA KATIKA MAFANIKIO.

Kila jambo lenye misingi katika ulimwengu huu hufungamanishwa katika misingi muhimu. Ipo misingi ambayo ukiifuata na kuifanya itakupeleka katika kilindi cha mafanikio. Mambo yafuatayo tukiyatilia maanani basi tutafanikiwa:


1. KUJITAMBUA (Self Discovery)

Kujitambua huja baada ya kujichunguza. Maisha ya mwanadamu hukamilika pale mwanadamu huyo kama atakuwa na tabia ya kujichunguza. Utambuzi binafsi huwasaidia watu kujielewa kuwa yeye, wewe au mimi ni nani?. Utambuzi binafsi wa mtu ni silaha kwa mtu mwenyewe ambayo humlinda mtu huyo dhidi ya tabiri zenye kukatisha tamaa toka kwa watu ambao wapo kwa ajili ya kuwakatisha tamaa wengine.

   Mfano; utawasikia wakikueleza kuwa '' Huwezi kufanikiwa kwa sababu katika familia yenu hamna aliyefanikiwa''. Kitu muhimu cha kuweza kukabiliana na kauli za kukupuuza na kauli hasi za watu wa namna hii ni kujitambua. Daima elewa kuwa '' Dunia imejaa watu weledi wa kukosoa na kukatisha tamaa wenzao kila wanapoinuka. Usiwajali 'Inuka na kuanza sasa'!.

2. KANUNI.

Tambua kuwa ''Daima maisha ni kanuni''. Kanuni ambazo ukizitumia lazima uelekee katika mafanikio. Kanuni hizi hutumiwa pia na waliofanikiwa daima nikiwemo mimi (ERICK SHIGONGO). Hebu chunguza mfano huu '' Taarifa (info) + Kufanyia kazi = Mafanikio.

Hivyo, chochote unachokisikia ama kuzungumzwa ni taarifa: Taarifa ambazo ukizitumia lazima mabadiliko uyaone. Kanuni hizi si mpya bali tunazo katika maisha yetu ya kila siku. Hujulikana kama SHERIA ZA MAFANIKIO. Kanuni hizi ni za kweli. Nizungumzacho ni kweli kwa maana mahali hapa nilipo (Erick Shigongo) kuna watu wanao nijua, wanao ijua familia yangu siku za nyuma enzi za uchumi mbaya.
Niliamua kuzitumia kanuni hizi kwa kufanya maagizo (taarifa) hakika nimeyashuhudia na ninaendelea kushuhudia mabadiliko katika maisha yangu na familia yangu kwa ujumla. Nami leo kwa kulitimiza kusudi la Mungu ninasimama mbele yenu kuwaeleza kuwa jamii yetu inahitaji watu waliofanikiwa. Haitafaa kitu katika nchi hii watu wachache watafanikiwa ilihali wengi wao hawakufanikiwa. Ili nchi yetu (Tanzania) iweze kuendelea katika nyanja kiuchumi na kijamii tabaka la kati lazima lifanikiwe. Lazima liwe na uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao utawezesha watu wengine kuajiriwa na kununua pia. Hivyo, nchi uliyopo ndio mahali sahihi kwako kufanikiwa. Unachopaswa kutenda ni wewe kujiamini. Kujiamini ni silaha katika kuelekea mafanikio. Kujiamini daima huleta mafanikio ambayo huanzia chini na si juu. Unapojiamini na kujenga hasira ya mafanikio ndani yako kuwa kwa nini yule alifanikiwa na mimi au wewe ushindwe. Kwa hiyo, kujiamini ni silaha ya kukupeleka katika mafanikio.

Tambua kuwa mtu awapo katika umaskini hupoteza kujiamini. Mfano halisi ni mimi Erick Shigongo, nikiwa darasa la tatu katika shule ya msingi Gedadi, Nyakato - Mwanza walikuwa wakiniita mjinga wa darasa. Hivyo, kutokana na umasikini ambao familia yetu ulipitia basi ulininyang'anya hali yangu yakujiamini darasani na hata nje ya darasa. Umasikini wa familia yetu ulinisababisha jina langu kupotea na kupewa jina la MADASA ambalo ni jina la Kisukuma lenye maana ya mtu mwenye kuvaa nguo zilizochanika.
Umasikini ulinidhalilisha, ulisababisha nipuuzwe mimi na wazazi wangu. Siku moja nikiwa na umri wa miaka kumi na minne nilikwenda kwa mara ya kwanza katika msiba wa rafiki yangu, ndipo niliposhuhudia wazazi wangu wakidhalilika kwa kukaa chini huku watoto wadogo wakiketi katika viti. Nakumbuka wazazi wangu walinifundisha kuwa kila nimuonapo mtu mkubwa amesimama nami nimeketi katika kiti au kigoda ni lazima nimpishe. Hali ile ilinitia uchungu moyoni nilimuuliza mama tukiwa nyumbani. Nililia mno kwa dharau ile kwa wazazi wangu. Mama alininyamazisha kwa sala ya baraka katika maisha yangu. Jifunzeni kuwafunza watoto wenu adabu njema. Hivyo, mambo hayo yalinitia hasira ya mafanikio kwa kauli za ndani yangu kuwa ''Nitamfanya kila mtu kuwa na adabu kwa wazazi wangu''.

3. KUWA NA UPENDO WA DHATI.

Upendo ni nguzo kuu katika maisha. Kuwa na upendo kwa watu wote, nchi yako na uudhihirishe upendo wako. Usiwe na kisasi kwani kisasi ni cha Mungu. Kwani kawaida ya Mungu kuwaleta mbele yako wale wote waliokutenda vibaya baada ya kufanikiwa ili uamue kuwasamehe au la.

'' Nakumbuka kijana mmoja aliwahi kufukuzwa kazi na mkuu wake kwa fitina ambayo ilitokana na utendaji kazi mzuri na elimu aliyokuwa nayo yule kijana. Hivyo, mkuu huyo alimfukuza kazi kijana yule kwa dhihaka na matusi. Baada ya miaka kupita naye alifukuzwa kazi akaanza kutafuta ofisi ya kukodi ili afungue ofisi yake. Siku moja alijikuta katika jengo refu ambalo alikuwa akimuuliza mhaziri (secretary) mara kijana yule aliyemfukuza alipita na akamuona kijana akipita. Alimuuliza mhaziri, huyu ni nani hapa? (kwa jazba) mhaziri alimjibu kwa upole: ''Huyu ndiye mkuu hapa na ndiye mwenye jengo hili''. Jamaa aliingia ofisini mikono ameweka nyuma alikwenda kumtaka radhi na kumwambia: ''Yaliyopita si ndwele tugange yajayo''. Hivyo, upendo kwa watu wote ni mojawapo ya njia katika mafanikio.

4. JIVUNIE KITU ULICHO NACHO.

Mtu bora katika dunia ni yule anayekionea fahari kitu alichonacho hata kama ni kikubwa au kidogo.

5. Tambua kuwa mafanikio yako katika maisha yatokane na hasira ya kufanikiwa, hivyo mateso au vitu ulivyopitia ndio nguvu itakayokusukuma kubadili maisha yako. Pia amini kuwa Mungu hashindwi kukuinua. Elewa kuwa Mungu anapomnyanyua mtu anamnyanyua kwa makusudi yake si kwa sababu wewe au mtu huyo ni mwema, la hasha! ni kwa sababu tu Mungu wetu ni mwema na ni mwaminifu.

Amini maisha unayoishi sasa ya taabu ni ya kitambo tu kwani yapo maisha mazuri mbeleni. Katika kipindi cha mwanzo lazima uwe mpole na mnyenyekevu mbele za Mungu. Mungu anaruhusu upite katika shida ili uwe na mizizi iliyokomaa, kimbunga kitakapokuja usitetereke wala kung'oka. Pia usikubali mwanao aitwe majina na wengine, jifunze kuwaeleza watoto wako habari za watu waliofanikiwa na umweleze uwezo uliomo ndani yake katika kuleta mabadiliko ya kimafanikio katika maisha.
Usiridhike na maisha uliyo nayo sasa piga hatua ubadilishe maisha na uwe na furaha.

HATUA ZA MAFANIKIO.

Ili tuweze kufikia mafanikio yatupasa kufanya na kujua kuwa:

UCHAGUZI > Mambo yote yamefichwa katika kuchagua. Kila unachokichagua ndicho upewacho. Kuna aina mbili za uchaguzi yaani uchaguzi bora na uchaguzi mbaya. Chaguzi bora matunda yake ni bora na chaguzi mbaya matunda yake ni mabaya. Hivyo jifunze kuchagua vilivyo bora katika maisha yako. Watu wengi watesekao sasa na wale walioteseka kale sababu kuu ya mateso yao walichagua vibaya. Ukichagua vyema utapuuza kubezwa. Hali ya kutojiamini itatoweka na utachagua kujiamini katika kila jambo utakalolifanya. Achana na kasumba mbaya kuwa wewe huwezi mbele za mzungu kwa sababu yeye ni mweupe au wewe ni mweusi. Achana na maneno ya uongo yanayosemwa juu yako.

Jifunze kutoka kwa kila mtu hata kama ni mjinga.

Usimruhusu mtu akuamulie kesho yako. Elewa kuwa kesho ni yako na Mungu wako, jifunze si kila kitu unachotaka kukifanya ni lazima umwambie mtu.

* Kuwa tayari kukubaliana na changamoto (Calculated Risk). Katika kuelekea mafanikio uwe tayari kukubaliana na changamoto zake. Pia epuka kuchukua muda mrefu katika kuandaa mambo yako. (Do be smart). Mpango mkakati si muhimu sana kwa sababu haukuelezi mambo mengi ya ziada.

* Chagua kuweka lengo katika maisha. Lazima uingie na lengo katika maisha yako. Ingia katika maisha ukijua wapi unakoelekea na lengo ndilo litakalokujenga wewe. Kama unataka pesa jiulize ni shilingi ngapi? Zije lini, tenga muda wa utekelezaji wa lengo lako.

-Jifunze kuweka lengo kubwa usiangalie uwezo ulionao wakati unapanga lengo lako. Achana na malengo madogo madogo. Elewa kuwa kama unataka kuwa si mtu wa kawaida basi malengo yako yawe ni makubwa. Tengeneza lengo kubwa kisha ligawe katika sehemu ndogo ndogo.
-Daima wenye malengo ndio wenye kuteseka.

* Chagua kupanga mipango.
Ukichagua lengo bila kupanga huwezi kufanikiwa. Tazama ulicho nacho na uanze nacho. Anza na ulicho nacho. Mungu hawezi kukupa wazo halafu akunyime msaada ila huwezi kupewa msaada na Mungu bila ya kuanza. Katika maisha ya kuanza mafanikio unahitaji mambo makuu matatu ambayo ni WAZO, WATU na FEDHA. Lakini vitu hivi vyote huwa haviji vyote kwa pamoja. Wanadamu ni wataalamu sana katika kuwaza lakini utekelezaji hakuna. Elewa kuwa kila kitu kinachofanyika duniani ni Mungu anafanya kupitia watu wake, weka mawazo yako ardhini ili yaonekane.
-Chagua ushindi kwa kila wazo unalopewa.

* Chagua Kutenda.
Ondoa woga na ufuate malengo yako uyatimize. Achana na kuogopa kufanya kuwa ukifanya ukishindwa utachekwa tambua kuwa hata usipofanya utachekwa tu. Fanya mpaka mwisho wako na Mungu atakuletea watu wa kukusaidia.
-Kuwa king'ang'anizi katika kutimiza malengo yako.
-Tambua kuwa kuna watu wana fedha zako ila anza kufanya ili ukutane nao

* Chagua kuwa mvumilivu.
Chagua kuwa mvumilivu, maisha ya mafanikio ya muda mfupi sio mazuri. Ukubali au kuwa mvumilivu hata unapokutana na changamoto. Maana mvumilivu hula mbivu daima, mafanikio yamo katika uvumilivu.

* Chagua kuwa na nidhamu ya pesa na wakati.
Hakuna mafanikio duniani bila kuwa na nidhamu ya muda na pesa. Elewa kuwa kila mtu duniani ana thamani, tambua kuwa kila unachokifanya kina thamani yake katika muda. Itambue thamani yako kwani kila mmoja ana thamani. Jiulize swali hili kuwa ''Unautumiaje muda wako/''. Watu wengi wanahusisha giza na usingizi bila kujua kuwa ni vitu viwili tofauti. Usiku pia ni muda mzuri wa kuweza kufanya jambo ambalo litakuingizia kipato. Tumia saa 24 kutengeneza fedha wewe mwenyewe au kupitia wengine (kuwaajiri).
-Heshimu fedha yako kwa kuudhibiti mkono wako. Jifunze tabia ya kuwa na nidhamu katika fedha hata kama huna jilazimishe. Wekeza fedha yako katika vyanzo vingine vya mapato.

* Chagua marafiki sahihi.
Uchaguzi wa marafiki walio sahihi watakupeleka mbele. Achana na marafiki wanaokuletea habari za matumizi ya pesa. Achana na rafiki ambaye unampa tu yeye hatoi. Maana urafiki ni kutoa na kupokea.

* Chagua watu unaotaka kufanana nao.
Chagua watu waliofanikiwa au unayemtamani kuwa kama yeye katika mafanikio.

* Chagua kujifunza.
Elewa kuwa kujifunza hakuna mwisho. Jifunze kila siku bila kusimama. Achana na tabia ya kuacha kusoma baada ya kumaliza shule au chuo. Soma vitabu mbalimbali vya ndani na nje ya taaluma yako kwa sababu hujui kitakachokuja kukuweka huru kifedha.

* Chagua kusaidia jamii baada ya mafanikio.
Tuna kila sababu ya kuwasaidia wasiojiweza. Msaidie mtu mwingine ainuke, hutafirisika.

MWISHO:
Hakika elimu bora hutoa watu bora katika jamii. Semina hii imewagusa wengi na kuwapa njia sahihi za kuinuka mahali walipokuwapo awali na kuelekea katika mafanikio.

MC. Harris Kapiga anaendelea kutumia alichonacho katika kuhakikisha Watanzania mbalimbali wanaishi maisha ya mafanikio tena bure kabisa. Karibu mpige hatua katika mafanikio, Ni Ndani Ya Ukumbi Wa Nchi Ya Ahadi, Sinza Kamanyola! ( 0713 059 959 )

Endelea kufuatilia Blog hii, Wiki hii nitakuletea kile alichosema Mkurugenzi wa CLOUDS MEDIA, RUGE MUTAHABA, usikose; amesema mambo mazito sana!

KUMBUKA: 
Kama ambavyo Blog hii imekuwa ikikuletea mafundisho yenye kubadilisha ufahamu/akili na maisha kwa ujumla; Unaweza kui-support Blog hii kwa kununua mafuta halisi ya alizeti yenyo ubora wa juu, Lengo ni kufanikisha Blog hii Iendelee kukuletea mafundisho mazuri kutoka kwa watu maarufu na waliofanikiwa ambao nimekuwa nao bega kwa bega ili kuhakikisha msomaji wangu anapata kitu kitakachoweza kumtoa hatua moja kwenda hatua nyingine!
   Ili kujipatia Mafuta haya waweza kuwasiliana nasi kwa  0659 700 002 na Mungu atakubariki.
Asanteni sana wadau wangu! 




Dream Big As You Grow Big.
0659 700 002, The Blogger!

PICHA ZINGINE ZA TUKIO





























Dream Big As You Grow Big.
mdee jr.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:


Juu