Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

JITAMBUE SAIKOLOJIA: JE MPENZI WAKO NI MWENYE HASIRA?

 

TAMBUA NINI CHA KUFANYA!

 
  By Chris Mauki, Mtaalamu wa saikolojia na jamii/mahusiano.

   Katika mahusiano ya aina yeyote hakuna  anayeweza kusema  hajawahi kukasirika.  Mara kwa mara tunakwazana na kukasirishana ingawa wako wale ambao hasira yao ipo karibu zaidi na huja  kwa ukali zaidi na mara nyingine huleta madhara katika vitu, watu, au hisia za mpenzi mwingine. 

Hapa nataka nikusaidie jinsi ambavyo unaweza kufanya pale mpenzi wako anapowaka hasira kali.  Kujua hili kutakusaidia kupooza  au kuponya hasira za mwenzako na sio kuchochea moto mkubwa zaidi ambao unaweza kuleta madhara makubwa zaidi. 

NINI CHA KUFANYA!
  1. Ikubali hasira ya mwenzako kama ndio njia yake ya kuonyesha hisia zake.
Hasira yake na kulipuka kwake kunaweza kuja kwa style ya kuleta  maudhi sana na  wala kusikokuwa na sababu ya msingi, lakini kubali kuwa ana haki ya  kuwa na hasira.  Hasira yake yaweza isiwe nzuri kwako lakini kumbuka haiashirii mwisho wa mahusiano yenu. Mahusiano yaliyo bora huruhusu kwa kiasi fulani vimikikimikiki kama hivi, huwezi kupinga visiwepo kwa asilimia 100.
 
  1. Mfanye mpenzi wako kuwajibika kwa hasira yake mwenyewe
Najua anaweza kukulaumu wewe kwa hasira zake, iwapo hali hii inatokea kataa kukubali wazo hilo, wewe hauhusiki kwa chochote, wala wewe sio sababu ya  hasira hizo bila  kujali  yeye anasema nini. Yeye ndio amechagua kukasirika na kufanya hivyo anavyofanya, na mara nyingi ni mbinu yake ya kukufanya ukubaliane na matakwa yake.  Kwa hali yoyote kataa kuchezewa kupitia hasira yake.
 
  1. Tulia na uwe na sababu ya kutulia kwako
Hata kama mpenzi wako kavuka mipaka kwa kukutukana, kukulaani, kukupayukia au hata kukupiga, bado waweza kuchagua kuwa mpole na mwenye sababu maalum ya kutulia kwako.  Taratibu na kwa upole mtulize kwa kumwonyesha uhalisia wa tukio.  Kwa busara na kujizuia kwa hali ya juu, jitahidi kumweleza mawazo yako, hisia zako na ukionyesha jinsi hali hiyo inavyokusumbua mara inapotokea, kamwe usitumie sentensi za “wewe” mfano “wewe unaudhi sana”, “Wewe sikuelewi kabisa” bali tumia sentensi za  “mimi”, mfano “mimi ninaumia sana unapofikia hali hii”.  Endelea kutoa mawazo yako kwa ufasaha na katika hali ya kumjali.
 
  1. Weka mipaka kwa hasira zisizo na sababu ya msingi
Kama mwenzako anazidi kuonyesha hasira yake isiyo na msingi, anatukana na kuendelea kubwatuka tu, na wala hakusikilizi unachotaka kukisema, basi unaweza kuamua kutoka  na kuwa pembeni ya eneo hilo, kwa upole mwambie kuwa utafurahi kuzungumzia  jambo hilo  mara atakapopoa ukali na  baada ya hapo nenda chumba kingine mpaka atulie.
  1. Jizuie usiombe msamaha au kumtaka radhi
Najua watu wengi, hususan jinsia ya kike wakifikia hatua hii hujiona wao ndio wakosaji na hivyo kukimbilia kuomba radhi.  Kumbuka kuwa mpenzi mkorofi na mtukanaji hastahili kuombwa radhi.  Ni kweli yawezekana  wewe ni sababu kwa kiasi fulani kwa tatizo hilo lakini kwa kule kukasirika kwa style hiyo hakumfanyi astahili kuombwa radhi maana kwa kufanya hivyo utaendeleza tabia yake hiyo mbaya.  Msamaha au radhi yaweza ikafaa baadae kidogo wakati mpenzi wako ametulia na ameiweza hasira yake. Jaribu kuihifadhi samahani yako mpaka wakati huo ufike.
 
  1. Mpongeze mpenzi wako mara tu anapoamua kufanya lile lenye staha na wala siyo anapoonyesha hasira.
Wakati wowote mpenzi wako anapoonyesha kushuka na kuelewakuwa analofanya sio jema, mpongeze, mtie moyo aendelee na tabia hiyo njema kwa kumwonyesha utayari wa kumsikiliza kile anachotaka kusema ili mfikie maafikiano. Katika mahusiano jifunzeni kuzipongeza na kuzitia moyo tabia na matendo mema na pia kuyazuia yale yasiyomema yasiendelee.
 
  1. Jipongeze Pia
Kamwe usiruhusu matukano, kejeli na kashfa za mpenzi wako zikuvunje moyo na kukushusha thamani yako.  Usijione mnyonge kwa lawama zake labda tu uchague kukubali anachokisema kwako.  Jione bado kuwa wewe ni mwema na ulikuwa unafanya mambo kwa nia njema.  Ukiweza jipongeze kwa kufanya kile ambacho hisia zako zitaona zimepongezwa.  Mfano, jitoe mtoko, nenda kwenye filamu, jipikie kitu kizuri, fanya nafsi yako ijisikie iko juu. Kama unajiona kuwa huwezi au unapata shida zaidi kuzifuata njia hizi basi jitahidi kumtafuta mshauri wa kisaikolojia “counselor” kwa msaada zaidi.
NAWASHUKURU WASOMAJI WANGU, SASA TUMEFIKIA WASOMAJI ZAIDI YA ELFU ISHIRINI NA NNE  24,000. ENDELEA KUTEMBELEA MARA KWA MARA NA KUWASHIRIKISHA WENGINE PIA.

Juu