Wakati dada Mary kutoka mkoani Arusha anaeleza kisa hiki kuhusu masuala mazima ya ndoa,
Mdee Junior (
Ze Blogger ) anajiandaa kwa engagement Jumapili hii ya tarehe 20 Jan. 2013 katika kanisa la
Ebenezer (
International Pentecostal Holiness Church ) lililopo Tabata Segerea. UNAKARIBISHWA KUMSINDIKIZA kijana huyu, kuwasiliana naye tumia mawasiliano hapo chini kabisa.
Sawa, baada ya utangulizi huo mfupi; hebu sasa jiweke tayari kusikia kile kinachojiri ndani ya wana ndoa hawa amabo ni Merian na Joseph ( sio majina yao halisi, kwa sababu maalum ).
NImejifunza jambo kutoka kwenye huu ushuhuda nadhani na wewe utapata kitu.
NAJUTA KWA NINI NILIKUBALI KUOLEWA!
Baada ya mwaka mmoja wa ndoa, Merian asema anajuta kwa nini alikubali kuolewa. Merian na Joseph (haya siyo majina yao halisi) ni mtu na mumewe. Nikiwa katika Mkoa wao kikazi, niliamua kuwatembela wanandoa hawa. Merian alinipokea na kunikaribisha ndani kwa furaha sana. Tukaanza kuongea nami nikamuuliza, Joseph yupo? Akaniambia bado hajarudi kutoka kazini, hata hivyo kaniambia yupo njiani anakuja.
Tukaanza kuzungumuza mambo kadha wa kadha na kisha nikamuuliza mnaendeleaje na ndoa yenu changa? Baada ya kuwa nimemuliza swali hili akacheka na kisha akaanza kwa kusema, nyie maisha haya ya ndoa yaacheni tu, kwa kweli najuta kwa nini nilikubali kuolewa? Kauli hii ilinishtua sana kwa sababu kwanza sikuitegemea na pia ndoa hii ilikuwa ndio imetoka kutimiza mwaka wa kwanza tu.
Kwa haraka kabla hajaendelea nikamzuia asiseme hayo maneno tena, maana nilijua kadri anavyosema ndivyo anavyozidi kuumba uharibifu kwenye ndoa yake. Akaniambia usinizuie, si umeuliza tunaendeleaje, subiri nimalize kukuelezea. Ndipo akaanza kuniambia kile kilichompelekea kusema anajuta kwa nini alikubali kuolewa (Kwa ufupi ni changamoto ambazo kwa ujumla naweza kusema za kawaida, hata hivyo sitaweza kuziandika hapa kwa sababu maalum).
Katika maelezo yake Merian aliniambia, vijana wengi sana walinifuata ili kunioa, mie nikawakataa, natamani ningeolewa na yoyote kati ya wale wengine, lakini si hapa nilipo na laiti likitokea lolote sasa (kwa maana ya mwenzake kufa) sitakubali kuolewa tena.
Mpenzi msomaji sijui kama unakiona ninachokushirikisha kupitia maisha ya wanandoa wenzetu hawa. Kumbuka ni mwaka mmoja tu wa ndoa, na leo tunashuhudia Merian akijutia maamuzi yake ya kuolewa na Joseph. Licha ya kwamba ni mwaka wa kwanza tu, lakini wawili hawa wameokoka pia.
Maelezo ya dada Merian yaliniletea maswali matano (5) ndani yangu ambayo ndiyo ninayotaka tujifunze kutoka kwake;
Swali la kwanza; Je! Merian, alijua nini maana ya ndoa kabla ya kuolewa?
Swali la pili: Je, Merian alijua aina ya maamuzi anayotaka kufanya kabla ya kuolewa?
Swali la tatu: Je, Merian alimuhusisha Mungu kabla ya kuolewa ili ampate mwenzi sahihi wa kuishi naye?
Swali la nne: Je, Merian alikuwa amejiandaa/andaliwa kifikra kuishi kama mke?
Swali la tano: Je, mpaka sasa, Merian anajua wajibu wake ni nini kwenye ndoa?
Kutokana na maswali haya niliwaza mambo matatu ambayo, nafikiri kama vijana wangefahamu yatawasaidia katika ndoa zao;
• Moja, ni vema vijana wajifunze kumshirikisha Mungu awaongoze kupata mwenzi sahihi wa maisha, kabla hawajaingia kwenye hizo ndoa.
• Mbili, ni vema vijana wakajifunza kufikiri kimapana kabla ya kuingia kwenye ndoa. Swali la msingi katika kufungua tafakuri hii, ni kwa nini mtu aoe au kuolewa? Ni swali fupi lakini kama wewe ni mtu ambaye hufikiri kimapana swali hili litakujengea msingi mzuri wa baadaye. Naam kile kitabu cha 1 Wakorinto sura nzima ya saba kikuongoze katika tafakuri hii.
• Tatu, ni vema vijana wangefunzwa/kuandaliwa vya kutosha kuhusu ndoa na hasa wajibu uliopo mbele yao. Endapo kama Serikali inawasomesha watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea uwezo na maarifa ya kutekeleza majukumu yao, basi ifike mahali kanisa, wazazi, viongozi wa vijana nk makundi haya yaone umuhimu wa kuwaandaa vijana wao kuyakabili maisha ya ndoa.
Watu wengi hufikiri chanzo cha matatizo kwenye ndoa zao ni Shetani. Ndio hii ni sababu moja, lakini sababu nyingine kubwa, ni watu wengi kukosa ufahamu wa masuala ya ndoa kabla na baada ya kuingia kwenye hizo ndoa. Naam wakati watu wanasema Shetani anaangamiza ndoa zetu, Mungu anasema, ndoa za watoto wangu zinaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6).
Ni imani yangu kwamba, kama mambo haya yatazingatiwa, sehemu kubwa ya changamoto ambazo wanandoa wanapitia, zingepata ufumbuzi wa haraka. Natoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya ndoa na hasa Wachungaji, Walimu na Viongozi wa makundi ya kiroho, kuanzisha utaratibu wa kuwa na mafunzo maalum kuhusu ndoa, kwa vijana ambao wameweka wazi dhamira zao za kuingia kwenye maisha ya ndoa.
Ni vema pia, hata kwa wale ambao wako ndani ya ndoa, wakawekewa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara, maana kwa mtazamo wangu ndoa ni shule ambayo, wahusika wanapaswa kuongeza (kujifunza) ufahamu wao kila siku, ili kulitumikia vema kusudi la Mungu.
Naamini umepokea kitu, kwako wewe ambaye bado hujaingia kwenye ndoa na wewe ambaye tayari upo kwenye ndoa! Haya ni mambo ya msingi sana kuyazingatia, na kwa sababu hiyo basi naomba mniombee sana maana najiandaa kuingia na engagement yangu ni jumapili hii tarehe 20. Jan. 2013 pale Tabata Segerea, karibu tushiriki pamoja.
Nitafurahi kukuona.
Mawasiliano:
+255 659 700 002
+255 756 145 417
mdeejunior@gmail.com (barua pepe)
@mdee_junior (twitter)
mdee.junior (skype)
DREAM BIG AS YOU GROW BIG.