Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO

MAMBO 7 AMBAYO MARA CHACHE SANA UTAAMBIWA AU KUYASIKIA KUHUSU MAHUSIANO/NDOA.


By Chris Mauki.
























1. Yamkini ipo siku utaamka katikati ya usiku wa manane na kumtazama aliyelala pembeni yako (ambaye labda unamuita au anajiita mpenzi wako) na kujiuliza “hivi maisha haya na huyu mtu ndo hadi kifo kweli?” (ukitamani walau kuwepo na kaupenyo kakutokea)

Swali hili linasababishwa na aina ya maisha mnayoishi, yamkini penzi mlilokuwa nalo awali haulioni au wote hamlioni tena, imebaki kuonekana tu na watu wa nje kama mnaopendana kumbe ukweli ni kwamba mnaishi tu pamoja “not as lovers but as in mates”. Zile zama za kuitwa jina lako la kwanza, na yale majina mengine kama darling, honey, sweet heart zimefia mbali na nafasi yake imechukuliwa na majina kama ‘mama nanihii’ baba naniii’ we nanihii’ eti nanihii’ eti wewe’!!! Ile ‘chemist’ au ule mvuto wa ndani ambao ulikuwa unausikia kutokea moyoni hadi katika mifupa yako mtu huyo akiwa karibu na wewe hauioni tena badala yake, akiwepo karibu ndio unaona bora awe mbali. Kipindi hiki mtu huyu akisafiri hutamani arudi, kila siku unamuuliza “unarudi lini eti?” sio kwa kusukumwa na hamu ya kutaka arudi mapema bali kwa kusukumwa na hamu ya kutaka kusikia yamkini kaongeza siku au amepata safari nyingine ya ghafla ili uendelee kufurahia kutokuwepo kwake.


2. Mara nyingine utajikuta inakulazimu kufanya kazi ya ziada kuliko uliyowahi kudhania katika kuhakikisha penzi lenu linasonga
Yamkini ulifikiri kuwa itakuwa rahisi mara ukikubali kuingia kwenye mahusiano na huyo mpenzi wako. Umetamani kuwa nae kwa muda, umemtafuta kwa muda na sasa ukafikiri mkiamua kuanza mapenzi pamoja ‘things will go smooth’. Mnakuja kugundua kuwa ninyi ni watu wawili tofauti, kila unachokipenda na kukitamani mwenzako hakithamini. Yale uliyokuwa ukiyaamini kama misingi ya mahusiano bora huyaoni kwenye mahusiano yako. Kila ulichowahi kukisoma, kujifunza au kuambiwa kuhusu kuyafanya mahusiano yawe paradiso unaona hakifanyi kazi kwenu. Matarajio yako makubwa kwenye mahusiano yenu na mustakabali wenu yanaingia ukungu na mbele yako huoni hata chembe ya mwanga. Sasa unajikuta ulichodhania ni rahisi kumbe sio, na unalazimika kujituma zaidi, kufanya kazi zaidi na kutumia muda yamkini kuliko mwenzako kuhakikisha mnaweka sawa mambo yenu ili angalau maisha yaendelee. Kuepuka hili nivema tunapoingia katika mahusiano tusiwe na matarajio makubwa kupitiliza na yasiyo tekelezeka ‘overambitious and unrealistic expectation’ Penzi peke yake ndilo litupeleke katika mahusiano kwa kiu ya kusaidiana kuhakikisha raha ya kila mmoja inawezeshwa, sio kwa kiu ya kutimiziwa kiu zako tu ‘this is ultimate selfishness’


3. Zipo nyakati unaweza kujikuta unaenda kitandani ukiwa na hasira, na yamkini ukaamka asubuhi ukiwa na hasira zaidi ya ulizo lala nazo.
Tofauti baina ya jinsia hizi mbili kama nilivyogusia kwenye jambo la pili ziko katika maeneo mbali mbali ya mahusiano yetu na mojawapo ni tofauti tulizonazo baina ya wanawake na wanaume hususani katika kuishuhulikia migogoro inayoibuka ndani ya mahusiano yetu. Yawezekana wewe ni mmoja wa wale wasio na hasira sana, muelewa, mwepesi wa kusamehe na kuchukuliana na hali, mara kwa mara unatamani mliongee jambo lililoleta utata baina yenu kabla halijakuwa kubwa na kuleta madhara. Tabia hii ni nzuri sana, lakini kwa bahati mbaya unakutana na mwenzako ambaye hakufunzwa vyema namna na jinsi ya kuishuhulikia migogoro. Unajua katika makuzi yetu wako ambao wamekuwa katika mazingira ambayo hayakuwaandaa kabisa kuja kuhusiana na bina damu mwingine yeyote, tabia zao wanazijua na kuziweza wao peke yao, ni ngumu hata kukaa na mtu huyu kwa lisaa limoja chini ya dari moja, katika saikolojia tunawaita “difficult personalities”. Unakuwa na mtu kama huyu kazini, kwa jinsi unavyoona tabia zake katika kuhusiana na wengine unajiuliza hivi mpenzi wake anaziweza vipi tabia zake? Sasa aina hii ya mtu unajikuta kwa bahati mbaya au nzuri labda ndio umehusiana naye katika mapenzi, kilasiku unategemea kuona mabadiliko lakini ndo maudhi yanazidi. Hata pale anapokuahidi kujitahidi kubadilika ili kukuridhisha bado unaona kama anaongeza machungu moyoni mwako. Kila siku unaona ‘bora hasira ulizokuwa nazo jana’. Ili kuepuka hali hii, kuwa macho sana wakati wa mahusiano, viko vitu vingi sana vya kuangalia katika tabia za mtu kabla hujaamua kuanza naye mahusiano ya kimapenzi. Hii habari yakujipa moyo na matumaini yasiyo rasmi eti ‘atabadilika tu!!’ ‘nitajitahidi kumrekebisha’…. ‘Mungu atambadilisha’ . Wengine wameshindikana tangia kwao tokea utoto we umekutana naye juzi tu utamuwezea wapi kama sio kujinunulia kitanzi kwa hela yako mwenyewe? Wako wengi waliotarajia hivyo hivyo kuwa wapenzi wao watabadilika sikumoja, bahati mbaya walipoamua kurasimisha mahusiano yao na wengine kuingia kwenye ndoa tabia ndo zikazidi kuwa mbovu na za kukatisha tamaa. “usijaribu kina cha maji kwa kuingiza mguu” Watch out.


4. Utakuja kugundua kuwa jitihada za kufanya mambo kivyako hazifanikiwi na sio muhimu kama pale ambapo mnaweka nia zenu pamoja.
Katika mikiki mikiki ya kushindana katika namna mnavyoishuhulikia migogoro yenu, yamkini baada ya kuona mambo hayaendi unaamua kujichukulia njia zako mwenyewe, humshirikishi mwenzako chochote, maamuzi yako ni yako binafsi na wala hutaki kusikia chochote kuhusu yeye. Yamkini ameamua kukuacha uendelee vile ulivyoona inafaa au labda bado hajakubaliana na uamuzi wako wa kujitenga na kuanzisha maisha binafsi ingawa bado mko chini ya dari moja. Katika yote haya utakuja kugundua mambo mengi hayaendi kiufanisi sana au labda yanatumia jitihada na nishati kubwa zaidi tofauti na pale ambapo yangehusisha nia zenu pamoja. Najua unaweza kusema ‘je kama hataki nimbembeleze hadi lini?’ lakini ukweli nikwamba usiwe na haraka ya kukimbilia kutapanya bali uwe zaidi na hamu ya kukusanya. Sio mambo yote yanarekebishika kwa usiku mmoja. Inabidi uifanyishe mazoezi misuli yako ya uvumilivu ili ikuwezeshe kustahilimi, ndani yako ukiwa na tumaini la kuuona mwanga na sio kiza. Kama wako waliowahi kuitafuta furaha iliyopotea na wakaiona, kwako pia inawezekana.


5. Mahusiano bora haimaanishi ni mahusiano yasiyo na migogoro wala mikwaruzano bali ni mahusiano ambayo wanaohusiana wameamua kuwatayari katika jitihada endelevu kuhakikisha kilakitu ndani ya mahusiano yao kinakwenda sawa.

Yamkini umewahi kudhani kwamba mahusiano bora ni yale ambayo mtajiepusha wakati wote na katika yote kuingia kwenye migogoro na mikwaruzano. Labda umewahi kujipanga kufanya hili mara uingiapo kwenye mahusiano au kutarajia hili toka kwa mpenzi wako na mara unapoona alama au dalili za migogoro basi unahisi kuwa uko katika mahusiano potofu nakutafuta njia za kujihadhari nayo. Napenda kukupa taarifa tu kwamba matarajio hayo ni matarajio hasi. Unahitaji kuya badilisha na kuwa na matarajio chanya yatakayo kuwezesha sio kukwepa na kuikimbia migogoro bali nyie wawili kwa pamoja kujua vyanzo vya migogoro yenu na namna bora itakayowawezesha kukabiliana nayo, kila mmoja akiwa na nia ya dhati na jitihada endelevu kuhakikisha mnalilinda penzi lenu dhidi ya kila pepo zitokazo ndani ya mahusiano yenu au nnje yake. Jitahidini wote kuwa na mtazamo huu kwasababu mara anapokuwa nao mmoja baina yenu inakuwa kazi sana pale ambapo mwenzako anaangalia suala la kutofautiana kwenu tofauti kabisa na wewe unavyoliangalia, na utaona matokeo yake pale mnapo tofautiana kwenye wazo au jambo fulani. Wakati wewe ukijitahidi kutafuta namna ya wote kusuluhisha na kuendelea mbele, yeye anakuhimiza kuwa mahusiano yenu hayakuwa mpango wa Mungu na kwahiyo kila mmoja atafute hamsini zake. Kwa tabia hii mtu kama huyu hawezi kamwe kutulia kwenye mahusiano bali anakuwa mtalii kutoka mbuga moja ya mahusiano kwenda mbuga nyingine, na wakati huo moyoni mwake kila mara akidhania labda mbuga inayofuata ni nzuri kuliko aliyopo.


6. Utakuja kugundua kuwa jitihada za kumbadilisha mpenzi wako kitabia zinakwama na kukuwia ngumu kuliko jitihada za wewe mwenyewe kubadilika.

Yamkini mlipokuwa mnaanza mahusiano au hata kabla hamjaamua kuanza mahusiano ulikuwa unaona baadhi ya tabia zake, nyingine hukuzipenda lakini kwasababu ya penzi ukazifumbia macho ukijipa matumaini zitabadilika mbele ya safari, au penzi litazifunika au labda utajitahidi kumbadilisha na kwasababu anakupenda atakubali kubadilika. Kwa bahati mbaya baada ya kupiga hatua za mapenzi mbele, kila unapoangalia mabadiliko ya zile tabia unaona hakuna kinachobadilika, na sasa hivi unashindwa kuzifumbia macho tena kama zamani, kila unapoziona unalazimika kuongea na kujibizana na kutaka akuhakikishie kuwa atabadilika. Yawezekana umeshaahidiwa mara nyingi tu “nakuahidi nitabadilika mpenzi” lakini wapi!!!! Ukijiangalia wewe ndio umekuwa kiongozi wakumbadilisha mwenzako kitabia, hadi akikuona anakuogopa kama mwanafunzi na mwalimu wake, tena mbaya zaidi ukute wewe ni aina ya wale ambao wakiona kosa hawalinyamazii hata dakika mbili hata kukiwa na wageni au marafiki, mtu anapewa vipande vyake ‘on the spot’. Bahati mbaya ni kwamba utajaribu sana kushindana na tabia zake hadi utakapo fikia uamuzi wa wewe kuangalia ni maeneo gani kwenye maisha yako ambayo ukijaribu kubadilika yanaweza kupelekea pia mabadiliko upande wa mwenzako katika hali chanya.


7. Kwa jinsi utakavyokuwa ukijitahidi kuzikabili hofu zako na changamoto nyingine katika kuyafanikisha mahusiano yenu ndipo utakapogundua uhalisi wa jinsi wewe ulivyo.

Maranyingine ni ngumu kujifahamu uhalisi wa vile ulivyoumbwa na jinsi tabia zako za asili zinavyojidhihirisha. Yamkini unadhani kuwa wewe ni mwema sana kumbe sivyo watu wakuonavyo nje. Tunaambiwa kwamba maranyingi mtu anapokamuliwa hadi tone la mwisho ndipo tabia yake halisi huonekana. Hali kadhalika katika mahusiano yetu ya kilasiku baina yetu na wale tunaowapenda. Labda unapicha fulani akilini mwako na unadhani wote wanakutazama hivyo, yawezekana ni picha nzuri au mbaya, wewe wajua. Ukweli ni kwamba kwa kadiri tunavyozikabili hofu zetu za kila siku katika mahusiano yetu na kwa jinsi tunavyokumbana na changamoto na kuzishuhulikia ndipo tunaujua uhalisi wa jinsi tulivyo, na pia ndivyo mwenzako anaweza kukusoma kinagaubaga namna na aina ya mtu anayehusiana naye. Kumbuka yamkini haya yasiwe matatizo bali changamoto tu.

                                        T-H-E E-N-D:
 
 
 




Juu