JITAMBUE SAIKOLOJIA:DONDOO ZA MSINGI KWA WALIOKO KWENYE MAHUSIANO - Part 1.
Majeraha ya moyoni mnayopandikiziana katika mahusiano yenu leo sio yote huisha kirahisi mara tu mnaposameheana na kuamua kuanza mambo yenu upya. Zipo nyakati hamna budi kulipa gharama ya vidonda na majeraha mliyoyaruhusu kutokea katika zile nyakati za ukakasi mlizopitia katika mahusiano yenu. Yamkini usilipe gharama ya maumivu leo lakini kesho ukaumia kwa kuwaona watoto wako wanapitia katika vitu vilivyosababishwa na mbegu ulizopanda wewe huko awali. Usisahau kuwa "what goes around comes around"
Heshima kwa mpenzi wako wa kiume inatakiwa kuota mizizi moyoni mwako bila shuruti na pasipo kuathiriwa na vitu kama uwezo wako wa juu kielimu, kiakili, uwezo wa kifedha, uwezo wa wazazi wako, mafanikio binafsi, uwezo wa kujuana na watu wenye uwezo "networks and connections" n.k. Katika mazingira haya ndipo mbegu ya unyenyekevu inapo ota na kumea.
Je unaishi nyumbani au kwenye nyumba? Unapotoka kazini au katika mizunguko unasema unaenda wapi... nyumbani au kwenye nyumba? Penzi na amani vinapokosekana baina ya waishio chini ya dari moja basi wanakuwa wanaishi katika nyumba "living in the house' bali penzi linapowajaa na kuwazunguka mahali hapo panaitwa nyumbani "home". Yawezekana we unapaita nyumbani kimazoea ila kiuhalisi ni kwenye nyumba. Tamani kuishi na kuwa nyumbani na watoto wako wakue wakiwa nyumbani.
Mapenzi hayamaanishi uwezo wa kumtafuta na kumpata mtu sahihi wa kuwa naye kwenye penzi bali uwezo wa kutengeneza mahusiano yaliyo bora na yenye utoshelevu baina ya walioko katika mahusiano hayo. Sio tu kwa jinsi gani umeanza mahusiano kwa penzi la nguvu na bashasha lakini zaidi ni kwa jinsi gani unalijenga na kuliongeza penzi lenu hadi mwisho.
Mara nyingi yako mambo ambayo tuliwahi kuyafanya au yaliwahi kutokea katika maisha yetu kabla ya mahusiano tuliyomo ambayo yamkini tunayaficha sana katika “history box” tukihofia kwamba kama yatajulikana kwa mpenzi wako basi yaweza kuleta mzozo mkubwa na yamkini kuwatenganisha kabisa. Hembu jiulize nini umewahi kufanya au kimewahi kutokea maishani mwako ambacho hujawahi kumwambia mpenzi wako na unahisi akikijua inaweza kuleta shida? Jiulize je unaijua “history box” ya mpenzi wako? Una tamani kuijua? au labda hata hutamani kuisikia maana itakuchafua na kukuhatarishia uwepo wako katika mahusiano yako? Wengine “history box” zetu ni majanga!!!! Kwahiyo tunatumia nguvu sana au hata garama kubwa katika kuzificha zisije kujulikana na wapenzi wetu. Mara nyingi inakuwa ngumu sana unapokuja kufahamu yaliyo kwenye “history box” baada ya kuzama kwenye mahusiano na kwa hivyo kukupa maumivu makubwa. Ni bora na vema katika urafiki na wakati wa kujuana kila mmoja akaweka bayana yaliyomo kwenye “history box” yake ili kila mmoja aamue kwa dhamira thabiti kuendelea au kusitisha safari ya penzi. Tatizo kubwa ni pale ambapo spidi ya kuingia kwenye penzi inakuwa kubwa na yenye upepo mwingi kuyafanya masikio na macho yako yasione wala kusikia kilichopo kwenye “history box” ya mpenzi wako. Unapofika ndani ukishatulia ndo unakuja kugundua kumbe “ulipokumbatia kwa mwili wote hapastahili hata kugusa kwa kidole”
Kule kujali kudogo sana tena kunakoonekana si kitu (katika macho ya mwanaume) huonekana ni kitu muhimu sana na kunakofaa kwenye macho ya mwanamke. Vitu vidogo, vinavyooneka havina haja hata ya kuvifanya (kwa mtazamo wa mwanaume) vimechukuliwa kama vinavyopendwa sana na kutamaniwa kufanyika wakati wote na jinsia ya kike. Katika mahusiano ni vema kufahamu kwamba sio mambo makubwa yenye tija na kuweza kukuza penzi bali mambo madogo. Wakati mwingine wala sio mambo makubwa huua penzi na kuwagawanya waliowahi kupendana sana bali ni mambo madogo. Yamkini kile usichokijali kufanyiwa wewe, mwenzako anakitamani sana umfanyie. Mara kwa mara tumekuwa tukikimbilia kwenye mambo makubwa tena yanayotugharimu pesa tukidhani kuwa kwa kuwafanyia hayo wapenzi wetu tunaongeza penzi kumbe viko vingine vidogo vidogo ambavyo hata havigharimu pesa, ila uthamani wake ni zaidi ya pesa. You better learn to touch the untouchable.
Chris Mauki
Mtaalamu wa Saikolojia Ya Jamii na Ushauri - UDSM.
0659 700 002 / 0653 100 100.
NAWASHUKURU WASOMAJI WANGU, SASA TUMEFIKIA WASOMAJI ZAIDI YA ELFU 25,000. ENDELEA KUWASHIRIKISHA NA WENGINE.