JITAMBUE SAIKOLOJIA: JE MPENZI WAKO NI MWENYE HASIRA?
TAMBUA NINI CHA KUFANYA!
By Chris Mauki, Mtaalamu wa saikolojia na jamii/mahusiano.
Katika
mahusiano ya aina yeyote hakuna anayeweza
kusema hajawahi kukasirika. Mara kwa mara tunakwazana na kukasirishana ingawa wako wale ambao hasira yao
ipo karibu zaidi na huja kwa ukali zaidi
na mara nyingine huleta madhara katika vitu, watu, au hisia za mpenzi
mwingine.
Hapa
nataka nikusaidie jinsi ambavyo unaweza kufanya pale mpenzi wako anapowaka
hasira kali. Kujua hili kutakusaidia
kupooza au kuponya hasira za mwenzako na
sio kuchochea moto mkubwa zaidi ambao unaweza kuleta madhara makubwa zaidi.
NINI CHA KUFANYA!
- Ikubali hasira ya mwenzako kama ndio njia yake ya kuonyesha hisia zake.
Hasira yake na kulipuka kwake
kunaweza kuja kwa style ya kuleta maudhi
sana na wala kusikokuwa na sababu ya msingi,
lakini kubali kuwa ana haki ya kuwa na
hasira. Hasira yake yaweza isiwe nzuri
kwako lakini kumbuka haiashirii mwisho
wa mahusiano yenu. Mahusiano yaliyo bora huruhusu kwa kiasi fulani vimikikimikiki
kama hivi, huwezi kupinga visiwepo kwa asilimia 100.
- Mfanye mpenzi wako kuwajibika kwa hasira yake mwenyewe
Najua anaweza kukulaumu wewe kwa
hasira zake, iwapo hali hii inatokea kataa kukubali wazo hilo, wewe hauhusiki
kwa chochote, wala wewe sio sababu ya
hasira hizo bila kujali yeye anasema nini. Yeye ndio amechagua
kukasirika na kufanya hivyo anavyofanya, na mara nyingi ni mbinu yake ya kukufanya
ukubaliane na matakwa yake. Kwa hali
yoyote kataa kuchezewa kupitia hasira yake.
- Tulia na uwe na sababu ya kutulia kwako
Hata kama mpenzi wako kavuka mipaka
kwa kukutukana, kukulaani, kukupayukia au hata kukupiga, bado waweza kuchagua
kuwa mpole na mwenye sababu maalum ya kutulia kwako. Taratibu na kwa upole mtulize kwa kumwonyesha
uhalisia wa tukio. Kwa busara na
kujizuia kwa hali ya juu, jitahidi kumweleza mawazo yako, hisia zako na
ukionyesha jinsi hali hiyo inavyokusumbua mara inapotokea, kamwe usitumie
sentensi za “wewe” mfano “wewe unaudhi sana”, “Wewe sikuelewi kabisa” bali
tumia sentensi za “mimi”, mfano “mimi
ninaumia sana unapofikia hali hii”.
Endelea kutoa mawazo yako kwa ufasaha na katika hali ya kumjali.
- Weka mipaka kwa hasira zisizo na sababu ya msingi
Kama mwenzako anazidi kuonyesha
hasira yake isiyo na msingi, anatukana na kuendelea kubwatuka tu, na wala
hakusikilizi unachotaka kukisema, basi unaweza kuamua kutoka na kuwa pembeni ya eneo hilo, kwa upole
mwambie kuwa utafurahi kuzungumzia jambo
hilo mara atakapopoa ukali na baada ya hapo nenda chumba kingine mpaka
atulie.
- Jizuie usiombe msamaha au kumtaka radhi
Najua watu wengi, hususan jinsia ya
kike wakifikia hatua hii hujiona wao ndio wakosaji na hivyo kukimbilia kuomba
radhi. Kumbuka kuwa mpenzi mkorofi na
mtukanaji hastahili kuombwa radhi. Ni kweli
yawezekana wewe ni sababu kwa kiasi
fulani kwa tatizo hilo lakini kwa kule kukasirika kwa style hiyo hakumfanyi
astahili kuombwa radhi maana kwa kufanya hivyo utaendeleza tabia yake hiyo
mbaya. Msamaha au radhi yaweza ikafaa baadae
kidogo wakati mpenzi wako ametulia na ameiweza hasira yake. Jaribu kuihifadhi
samahani yako mpaka wakati huo ufike.
- Mpongeze mpenzi wako mara tu anapoamua kufanya lile lenye staha na wala siyo anapoonyesha hasira.
Wakati wowote mpenzi wako anapoonyesha
kushuka na kuelewakuwa analofanya sio jema, mpongeze, mtie moyo aendelee na
tabia hiyo njema kwa kumwonyesha utayari wa kumsikiliza kile anachotaka kusema
ili mfikie maafikiano. Katika mahusiano jifunzeni kuzipongeza na kuzitia moyo
tabia na matendo mema na pia kuyazuia yale yasiyomema yasiendelee.
- Jipongeze Pia
NAWASHUKURU WASOMAJI WANGU, SASA TUMEFIKIA WASOMAJI ZAIDI YA ELFU ISHIRINI NA NNE 24,000. ENDELEA KUTEMBELEA MARA KWA MARA NA KUWASHIRIKISHA WENGINE PIA.