IKIWA LEO NI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI; MWANAMKE HUYU ASEMA: ''NATEMBEA NA BARUA YA KIFO MKONONI''
Hali hii ndiyo iliyomkuta Veronica Kibuga (85)
mkazi wa Kitongoji cha Kahangala wilayani Magu, Mwanza ambaye kwa miezi
kadhaa amekuwa akiishi kwa hofu kwani anasubiri utekelezaji wa ‘adhabu
ya kifo’ kukatwa kwa mapanga kutokana na tuhuma kuwa yeye ni mchawi.
Ujumbe uliotumwa kwake uliandikwa kwa lugha ya Kisukuma na
ulikutwa kisimani ambako waliupeleka walipokwenda kuteka maji na
unasema: “Bamayo yashikaga izamu igawo ya kukatwa mapanga”, ukimaanisha:
‘Imefika zamu yako ya kukatwa mapanga’.
Majirani wamejaa nje ya nyumba ya Kibuga kwani
wanafahamu fika kwamba mwandishi wa ujumbe ule hatanii, kwani wote
waliowahi kupata ujumbe kama wake waliuawa. Huyu ni mmoja, lakini ukweli
ni kwamba wanawake wengi, hasa wazee wanaishi na makovu na wengine
wamepoteza maisha baada ya kupokea taarifa kama hizi.
Wakati dunia nzima ikisherekea Siku ya Mwanamke
Duniani leo hii, wanawake wa aina ya Kibuga wako ndani wamejifungia
wakihofu usalama wao kutokana na kuishi katika jamii ambayo inamwona
kama mkosi na chanzo cha matatizo yote.
Wanawake wanasherehekea leo na kutukuzwa kwa
mchango wao mkubwa katika masuala mbalimbali, lakini wapo wanaohitaji
ukombozi ili watoke kwenye madhila ambayo yamewafanya kuishi kwa
wasiwasi mkubwa.
Hata watoto wadogo wanapofariki, huwa inaaminika
kuwa mwanamke mchawi ndiye ‘aliyemla nyama’. Dhana hii imewafanya baadhi
ya wanaume vijijini kuwaachia wanawake kazi ya kuchimba makaburi.
Haya ndiyo yaliyomkuta Kibuga ambaye leo hii anatembea na waraka wa kifo mkononi, akisubiri ‘siku ya hukumu yake’.
Simulizi yake
Kabugu anasema: “Siku moja niliamka asubuhi na
kukuta majirani zangu wakiwa nje ya nyumba yangu, walikuwa wameniletea
ujumbe wa kifo kutoka kwa mtu asiyejulikana akisema ataniua mimi na
watoto wangu kwa kuwa ni wachawi.”
Barua hiyo iliyotumwa na mtu anayejiita ‘Meneja wa Kujiajiri’ ilieleza kuwa Januari 30 atafika katika nyumba ya bibi huyo na kummaliza kwa kumkata mapanga yeye na familia yake.
Watoto wa Veronica ambao ni Usia na Magdalena Kibuga nao wametajwa kuwa watauawa pamoja na mama yao kwa kuwa wanasaidiana naye katika masuala ya uchawi.
“Nimekuwa na hofu ingawa tarehe yenyewe imeshapita. Ninaogopa
kwa sababu wenzangu wengi wamewahi kupata barua kama hizi na kupigwa kwa
mapanga mpaka kufa,” alisema Kabuga.
Akizungumzia ulipoanzia mkasa huo anasema analihusisha tukio hilo na kugombea mashamba ambayo aliachiwa na marehemu kaka yake.
“Siku moja nilikuwa shambani nikilima ‘majaruba’ ya
mpunga, alikuja mtoto wa marehemu kaka yangu na kuniambia niache kulima
hapo kama sitafanya hivyo atanikatakata kwa mapanga. Ninahisi atakuwa
ameamua kunizushia tuhuma za uchawi ili niuawe,” alisema Kabuga.
Alisema tishio hilo limemuathiri yeye na familia
yake kwani wanashindwa kuendelea na shughuli za kilimo, wakihofu huenda
mtu huyo anaweza kuwavamia shambani na kuwakata kwa mapanga.
“Tangu wakati ule imebidi tuishi katika nyumba
moja, mimi pamoja na watoto na wajukuu zangu tunalala katika nyumba moja
ili kujilinda. Hali hii imetufanya tushindwe kuendelea na shughuli zetu
za kila siku,” alisema.
Watoto wake
Akizungumzia tukio hilo, Magdalena alisema wanaishi katika hali ya kukata tamaa kwani inavyoonekana Serikali imeshindwa kuwalinda, hivyo hatima yao ni kifo tu.
“Tumeamua kuishi pamoja na mama
ili hao wauaji wakija watumalize tu, hatuwezi kufanya chochote na watu
hawa inaonekana wameshindikana kabisa,” alisema Magdalena na kuongeza:
“Kwa miaka mingi haya matukio yamekuwepo, kama
wenzetu wanauawa kila siku unafikiri sisi tutapona? Tunajua ipo siku
watakuja tu kutukatakata lakini ukweli sisi siyo wachawi na wala
hatuujui. Tunachoamini hawa wauaji wanakuwa na sababu nyingine tu.”
Uongozi wa Kitongoji
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Mathias Ombesa
alisema juhudi zinafanywa kuwalinda wanawake hao hata hivyo anakiri kuwa
ni vigumu kutokana na mazingira halisi.
Ombesa alisema kutokana na wanawake hao kuishi
katika nyumba ambazo milango yake ni ya kusukuma, hurahisisha kazi ya
wahalifu katika kutekeleza maazimio yao.
“Kama unavyoona nyumba moja ipo hapa na nyingine iko kule mbali,
siyo rahisi kuifikia hata unaposikia mtu akiomba msaada na utakapofika
pale, utakuta mhalifu ameshatekeleza azma yake. Pia kama nyumba angalau
ingekuwa na mlango imara ingesaidia kuwafanya hawa wahalifu wasiingie
kwa urahisi,” alisema Ombesa.
Akizungumzia sababu za kushamiri kwa matukio kama
hayo alisema kwamba mila na desturi bado zinamkandamiza mwanamke kwa
kumhusisha na matukio ya uchawi baada ya kuzeeka.
“Hapa watu wengi wanaamini wazee wanawake ndiyo wachawi. Mfano mtu anapokuwa na mtoto wake mgonjwa, bibi
kizee akimtajia dawa na akapona, moja kwa moja humuhusisha na uchawi na
hoja yake huwa, kama ameweza kumponya mtoto basi anaweza kumroga,”
alisema Ombesa.
Akizungumza mratibu wa Shirika la Maperece
linalojishughulisha na kampeni ya kupunguza mauaji ya vikongwe wilayani
Magu, Athanasio Kweyunga alisema umaskini ni chanzo cha mauaji hayo kwa
kuwa hakuna tajiri ambaye huhisiwa kuwa mchawi.
“Umaskini unawaathiri wanawake, kwa mfano
anapopikia kuni kwa muda mrefu macho yake huwa mekundu. Pia wajane
huishi katika nyumba mbovu kutokana na kuwa na uwezo mdogo,” alisema
Kweyunga.
Aliongeza kuwa kupungua kwa ardhi kutokana na
ongezeko la watu ni sababu nyingine inayoongeza mauaji hayo, huku
akisema kuwa wanachofanya ni kuwaelimisha vijana namna ya kuitumia ardhi
ndogo wanayorithi kutoka kwa wazazi wao.
“Uchunguzi tuliofanya, tumegundua kuwa mauaji
mengi yamekuwa yakifanywa na wanafamilia na chanzo huwa ni kugombea
ardhi au mifugo. Vijana wanataka kumiliki sehemu kubwa ya ardhi na njia
pekee ya kuipata ni kuwaua wazee,” anasema Kweyunga.
Alisema shirika hilo linawaelimisha vijana pia
kuwawezesha wazee ili kuondokana na umaskini ambao huwafanya wahusishwe
na imani za uchawi.
Chikawe anena
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe
alisema Serikali italifuatilia suala hilo na kutoa ulinzi kwa watu
waliopewa vitisho.
Aliongeza kuwa anawaomba wananchi hao watoe ushirikiano kwa askari ili kusaidia juhudi za Serikali katika kukomesha mauaji hayo.
“Kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao,
nitasimamia kuona wanawake hao na wengine wanalindwa dhidi ya ukatili wa
aina yoyote. Ninawaomba wananchi wasaidie katika kutoa taarifa ili
watuhumiwa wafikishwe mbele ya sheria,” alisema Chikawe.
Source:
Mwananchi.
Source:
Mwananchi.