RIWAYA : JINAMIZI LA MABINTI
MTUNZI: ELIA MWAIPOPO
SEHEMU YA 1
KWA WASOMAJI WAPYA
Hadithi hii ni ya kubuni tu, lakini yenye kueleza uhalisi wa maisha na mambo yafanyikayo hasa kwenye ulimwengu wa roho (spiritual realm) na ule ulimwengu wa damu na nyama (physical realm), majina yaliyotumika hayana uhusiano wowote na watu wenye majina kama hayo …
Jinamizi lisilojulikana kwa kipindi kirefu, limeendelea kuwakumba mabinti wengi vigori kwa njia za kishirikina pasipo wao kujitambua. Mabinti hao licha ya kuwa na mvuto mkubwa mbele ya vijana watanashati wanafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuziteka hisia zao na kujikuta wakishawishika na kujiingiza katika mahusiano ambayo yanahatarisha maisha ya vijana hao kwa muda mrefu. Usiri mkubwa unatawala katika vifo hivyo vya kusikitisha hali inayopelekea kuibuka kwa hofu kubwa katika jamii….Hadithi inaanzia kwa msichana Monica, usiku wa manane huku akiwa kitandani anashituka na kuanza kushuhudia maruweruwe mengi, kwa taharuki kubwa anaamkaa na ……ENDELEA
******************************
Yapata majira ya saa nane za usiku, Monica anashituka ghafla akitokea usingizini alikokuwa amelala na kuanza kuona matukio ya ajabu machoni mwake, ghafla anahisi nywele zikimsisimka na kuanza kutetemeka, haukupita muda kijasho chembamba kinaanza kumtiririka usoni kwake hali iliyoambatana na hofu kubwa inayoyabadili kwa kiasi kikubwa mapigo ya moyo wake na kuyafanya yawe na kasi zaidi.
******************************
Huku haya yakiendelea Monica anahisi kupata hisia juu ya kile kilichokuwa kikiendelea lakini asijue nini cha kufanya. Anachungulia dirishani huko nako anapokewa na kiza totoro kilichosheheni weusi mithili ya mkaa. Taharuki inazidi kuukumba moyo wa Monica pale anapohisi joto na baridi vikiongezeka mwilini mwake kwa pamoja.
******************************
Zinapita dakika kumi na tano huku akiwa ameduwaa anajaribu kujitafutia msaada kwa kupiga yowe kubwa ambalo linakuwa halina maana yoyote kwani halikuwa likisikika na mtu yeyote aliyekuwa karibu na chumba chake. Kufumba na kufumbua macho Monica anajikuta yuko ndani ya kifuu mithili ya kile cha nazi kwa udogo na na taratibu anapaa kuelekea asikokujua huku joka kubwa likiwa limezunguka kingo za kifuu hicho ambacho kwa wakati huo kilikuwa kikipaa taratibu.
******************************
Wakati hayo yakitokea joka lilikuwa likitema moto wa cheche za kijani kuelekea machoni na kuzitisha mboni za Monica binti ambaye alikuwa akisifika kwa uzuri na sifa kem kem. Ndiyo ulikuwa ni msafara mkubwa uliokuwa ukiongozwa na Madubwana ambayo ni maarufu kama Majitu yaliyokuwa na sura za kutisha ambapo yalikuwa na macho matatu na pembe tatu..Juu ya mboni zao Madubwana hayo inasemekana kulikuwa na machipukizi ya viganja mithili ya vile vya binadamu na inasadikika kuwa hali hii ilitokana na mahusiano yao ya hapo zamani yaliyokuwepo baina ya Madubwana hayo na binadamu wa kawaida ambapo inasemekana uhusiano wao uliharibiwa na Madubwana pale yalipoanza kuwakamata na kuwala binadamu.
******************************
Wakati Monica akifikiria namna ya kujinasua akajikuta akipokea amri yenye vitisho ambayo ilimuamuru kutokugeuka wala kupiga kelele “Usigeuke wala kupiga kelele, achama mdomo wako ili tuingie na tujihifadhi kwa miaka ijayo” kisha amri hiyo ikafuatiwa na kicheko cha dharau “aaaaaaahaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa
******************************
Ilikuwa ni safari ya kuelekea angani liliko anga la kaskazini ambako inasemekana na kuaminika na wengi kuwa huko ndiko viumbe wengi na wa kila aina wenye kustaajabisha walikimbilia huko baada ya mifarakano mikubwa kutokea duniani yakiwemo Madubwana na viongozi wao. Awali, kabla ya Majitu kuja duniani na kumnyakua Monica palikuwa pametokea balaa kubwa sana la njaa hali iliyopelekea Madubwana mengi kupoteza maisha. Inasemekana takribani miaka saba Majitu yalikosa kabisa chakula na maji, mwanzoni katika kutatua tatizo hilo majitu yalianza kukamatana yenyewe na kulana kama chakula na wakati mwingine yalilazimika kukamata madubwana mazee ambayo yalikuwa dhaifu na kuanza kuyala kama chakula. Hali hii ilisababisha majitu kupungua kwa kasi kubwa sana.
******************************
Inaaminika baada ya madubwana mazee kuisha Madubwana yalianza kupunguza sehemu za viungo vyao na kuvifanya kama chakula chao. Mikia yao ambayo ilikuwa imenona mafuta na pembe zilizokuwa kavu mithili kuni zilizokaukia juani kwa kipindi kirefu nazo ziligeuka na kuwa msaada mkubwa sana kwa madubwana hayo. Habaari za taabu na kutaabika kwa majitu hayo zilimfikia kiongozi wao ambaye kwa wakati huo wala hakuwa na habari juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwani yasemekana ilipokuwa ikikaribia majira ya kipindi cha joto Kiongozi huyo maarufu kwa jina la Iisambo alishuka duniani na kuyaendeleza maisha yake yaliyoshabihiana kwa karibu kabisa na majini walioko duniani. Tofauti yao ilikuwa wakati majini walioko duniani walikuwa wakiishi kwa kunyonya damu binadamu na viumbe wengine, Irisambo aliishi kwa kutegemea nyama za binadamu na viumbe waliokuwa wakiishi katika dunia ya tatu.
Kwa kuwa hali ilikuwa ni tete katika anga hilo la kaskazini Irisambo siku moja aliitisha kikao kilichodumu kwa takribani masaa kumi na mbili akitafakari kwa kina kiini cha matatizo yake na suluhisho la matatizo yaliyokuwa yakiwakabiri madubwana hayo. Katika kutafuta suluhisho hilo akaja na mbinu ambazo kwa fikra za kijitu Irisambo aliona ni njia mbadala wa kutatua tatizo hilo………..ITAENDELEA
******************************
******************************
SHARE &COMMENT
ITAENDELEA JUMATANO 24/07/2013