Tamko la Serikali Kuhusu Mauaji ya Watanzania Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, amesema leo kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa katika mashambulizi dhidi ya wageni huko Durban na Johannesburg nchini Afrika ya Kusini.
Mhe. Membe amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Watanzania watatu wameuwawa katika mashambulizii hayo siyo za kweli.
“Nimehakikishiwa na Waziri wa Usalama wa Afrika kusini, David Mahlobo, asubuhi hii kuwa hakuna Mtanzania kati ya watu wanane waliouwawa, ambao ni raia wa Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland,” ametaarifu Mhe. Waziri.
Amesema serikali ina taarifa kuwa kuna Watanzania watatu waliofariki dunia nchini Afrika Kusini, lakini hawakuuwawa katika mashambulizi ya wenyeji dhidi ya wageni.
“Watanzania hao ni Rashidi Jumanne, ambaye imetaarifiwa alipigwa risasi katika tukio la ujambazi, kilometa 90 nje ya mji wa Durban; mfungwa Athumani China Mapepe, aliyeripotiwa kuchomwa kisu gerezani wakati wa vurugu za wafungwa, na Ali Heshima Mohamed, ambaye alifariki hospitalini kutokana na ugonjwa wa TB,” alieleza Mhe. Membe.
Mwili wa marehemu Mohamed ulirejeshwa nchini jana kwa mazishi. Mhe. Waziri alitaarifu kuwa kuna Watanzania 23 katika kambi iliyotayarishwa na serikali ya Afrika Kusini huko Durban kuhudumia wageni wanaokimbia mashambulizi hayo ya wenyeji, na kuwa utaratibu unafanywa kuwarejesha nyumbani raia 21 walioomba. “Wawili wamesema hawako tayari kurudi.”
Mhe. Membe amesema taarifa ya serikali ya Afrika Kusini inaonyesha kuwa hali ya utulivu imerejea Durban na Johannesburg katika saa 48 zilizopita kutokana na juhudi za Rais Jacob Zuma na kamati maalum ya mawaziri aliyoiteua kushughulikia mashambulizi hayo.
Mapema jana, Mhe. Membe alimwita Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Thamsanqa Dennis Mseleku, na kuelezea kukerwa kwa serikali na mauaji ya wageni na akataka hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha usalama wa Watanzania nchini Afrika Kusini.
Alisema Tanzania inaunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambayo imelaani vikali mashambulizi ya Waafrika kutoka nje ya Afrika Kusini. Hata hivyo, Rais Mugabe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), amesifia hatua zinazochukuliwa na serikali ya Afrika Kusini kukomesha mashambulizi hayo na kurejesha utulivu.
Mhe. Membe aliwataka Watanzania waishio Afrika Kusini na kwingineko nje ya nchi, kujitambulisha kwenye balozi zetu ili iwe rahisi kufuatilia usalama wao na kuwasaidia pale yatokeapo majanga.
“Hatuna takwimu sahihi za idadi ya Watanzania waishio Afrika kusini kwa sababu wengi wao wamekwenda huko kwa njia za panya,” alisema. Inakadiriwa kuna Watanzania 10,000 waishio Johannesburg na Durban.
Akijibu swali la mwandishi wa habari, Mhe. Membe alisema Tanzania inapaswa kutumia utajiri mkubwa wa gesi asilia ilionao ili kuendeleza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vitakavyotengeneza ajira za kuvutia kwa vijana ili wasikimbilie nchi za nje na kuhatarisha maisha yao.