RIWAYA: JINAMIZI LA MABINTI
MTUNZI: ELIA MWAIPOPO
SEHEMU YA PILI (2)
ILIPOISHIA SEHEMU YA (1)
Kwa kuwa hali ilikuwa ni tete katika anga hilo la kaskazini Irisambo siku moja aliitisha kikao kilichodumu kwa takribani masaa kumi na mbili akitafakari kwa kina kiini cha matatizo yake na suluhisho la matatizo yaliyokuwa yakiwakabiri madubwana hayo. Katika kutafuta suluhisho hilo akaja na mbinu ambazo kwa fikra za kijitu Irisambo aliona ni njia mbadala wa kutatua tatizo hilo.
ENDELEA…………….
Wakati mkutano huo ukiendelea Irisambo mkuu wa Majitu yote katika anga la kaskazini , aliyekuwa ameketi kwenye kiti kikubwa kilichokuwa kimetengenezwa kwa Mifupa ya viumbe mbalimbali waliokuwa wakipatikana duniani, pembeni yake alikuwa ameketishwa Monica msichana mrembo ambaye kwa wakati huo alikuwa hajitambui. Kihisia aliyavutia majitu mengi kama kitoweo huku mengine yakimtamani kimapenzi. Baada ya muda mrefu kupita Irisambo alichukua kiganja chake na kumpiga kofi dogo Monica hali iliyomfanya Monica aanze kurejewa na fahamu zilizokuwa zimepotea kwa muda wa siku saba. Aliporejewa na fahamu Monica alijikuta amezungukwa na Majitu yaliyokuwa karibu kabisa na mboni za macho yake huku akiwa ameketi kwenye fuvu la kichwa cha mtoto mchanga. Miguuni alihisi kama amebebeshwa gunia la mawe ile hali alikuwa akiona utepe mdogo wa kamba nyeusi mithili ya nywele za binadamu zikiwa zimefungwa kila mguu wake.
Alipogeuka nyuma alisikia sauti ya Irisambo akiyaagiza Majitu kuwa “ kuanzia leo ni marufuku kwa Majitu kulana wenyewe kwa wenyewe, tumepata suluhu ya matatizo yetu, binadamu hasa wasichana mabikira wanaoaminika kupendwa na wanaume wengi duniani wanaweza kutatua shida hii ya ukosefu wa chakula unaotukabili. Irisambo akaendelea, Majitu yanatakiwa kuwaingia wasichana hawa ili kurahisisha shughuli nzima ya kuwakamata kirahisi wanaume wa duniani ambao watakuwa wakinasa kwa mabinti hao wazuri na ambao bado hawajauharibu usichana wao.
Monica hapa atashushwa duniani na atakuwa msichana wa kawaida licha ya kumpa nguvu zetu za ulimwengu wa Ki-irisambo na kwenda nazo duniani ambako atawaambukiza wasichana wengine mabikira walioko sehemu mbalimbali za dunia hali ambayo itarahisisha upatikanaji wa chakula chetu kiurahisi”, wakati hayo yakisemwa na Irisambo alipofika mwisho Majitu kwa furaha yakaruka ruka juu na kujibu kwa pamoja Ndiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii
******************************
Dakika mbili baadae radi kubwa ikamulika kuelekea katika kiti alichokuwa ameketi Monica, haukupita muda akajihisi kuwa na nguvu za ziada huku mwili wake ukijaa misuli mikubwa iliyotutumuka kila sehemu ya mwili wake. Baada ya muda kupita Monica akajikuta akitapika vipande vipande vya mabonge ya damu iliyokuwa imeganda .Haukupita muda kabla ya Irisambo kuliita Jitu moja na kulikata sehemu ya mkia wake na kitu chenye ncha kali hali iliyosababisha kuruka kwa damu nyingi sana ambayo ilikuwa ikimuelekezea Monica katika sehemu aliyokuwa ameketi, Monica akaamuriwa akaifyonze damu ile iliyokuwa na rangi nyeusi zilizokuwa zimechanganyika na wekundu uliofifia. Monica alipomaliza kufanya tukio hilo Irisambo na Madubwana yalishangilia kwa nguvu sana yakiashiria mwisho wao wakumfanya Monica binti aliyekuwa mrembo na ambaye usichana wake haukuharibiwa na wanaume wa duniani kufanana na Majitu. Shangwe zikaendelea wakati ambapo Monica alikuwa ameshapoteza fahamu mara tu baada ya kuanza kuinyonya damu iliyokuwa mkiani kwa Jitu hilo.
Siku saba tena zilihitajika kwa Monica kuwa mfu wa muda ambapo alipotezwa tena fahamu kwa mara nyingine tena lakini safari hii akirejea Duniani kuja kukamilisha kazi aliyokuwa amepewa na Irisambo mkuu wa Majitu yaishiyo katika anga la kaskazini.
Siku ya saba akashushwa duniani akiwa ni binti tofauti na Yule wa zamani, ambapo yasemekana uzuri wa macho yake angavu na kidevu kilichochongoka kwa ustadi mkubwa vilizidi kuwa kivutio kikubwa kwa wasichana wenzake, hali kadhalika wanaume pia ambao siku zote walikuwa wakitamani kuwa na binti huyo mrembo. Alikuwa ana kiuno cha mduara kilichobinuka mithili ya kichuguu, ngozi yenye ulaini na unadhifu ulishikamana sambamba na uasili wa nywele zake. Kwa vijana wengi safari hii alipewa jina la “ Maria Cleopatra” (mwanamke anayeaminika kuwa ndiye mwanamke aliyewahi kuwa mzuri kuliko wanawake wote ulimwenguni).
Kitu kikubwa na cha kushangaza ni kwamba Monica hakuonewa wivu na wasichana wenzake tu bali hata wavulana pia. Kwa kawaida haikushangaza kusikia minong’ono kuwa binti huyu alikuwa akijisikia au (kuwa na mapozi) kama wasemavyo vijana wa siku hizi waliokulia mijini. Kuhusu mwendo wake mara nyingi ulizua taharuki kubwa na mihemuko ya kihisia kwa vijana makapela na wazee hali iliyohamisha hisia zao huku wengi wakihisi wapo dimbani wakisakata kabumbu na binti huyo. Utanashati sifa yake kuu kwani tangu udogo wake hakuwahi kukutwa na matope wala kuvaa nguo kuu kuu, licha ya kuwa na maisha ya kwaida katika familia ya Mzee Wazza Likuhusulo.
*********************
Si kila king'aacho ni dhahabu.... Tafakari kabla hujachukua maamuzi ya kupenda/mshirikishe Mungu kwanza.
ITAENDELE
KUMBUKA KUKOMENT, SHARE & LIKE.
Toa comment zako hapo chini palipo andikwa Comment.
Asante kwa kuwa mfuatiliaji mzuri..........