Chat Now

HABARI MPYA

FUNDISHO LA MSINGI

PICHA NA MATUKIO

CAPACITY BUILDING CLASS

MAHUSIANO

NUKUU YA LEO


   Mdee, mtumwa wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima na uponyaji wa nafsi, roho na mwili ulio katika Kristo Yesu; kwa msomaji mpendwa wa Blog hii. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu aliponiita hata wakati huu ninapokuletea fundisho hili litakalokutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine (from glory to glory), kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana ili ujae furaha. (FURAHA YA BWANA NDIO NGUVU ZETU ).

   Katika fundisho hili FURAHA NGUVU YA MWAMINI napenda tuangalie mambo machache ya msingi.

1. NINI MSINGI WA FURAHA YETU KATIKA KRISTO?
2. MBINU YA KIVITA
3. JE KUFURAHI NI SUALA LA KUJISIKIA?
4. JE MAJARIBU NI MKOSI?
5. NI JAMBO GENI KUINGIA KATIKA JARIBU?
6. JE NI JAMBO LA KIUNGU/KIBIBLIA KUFURAHIA UDHAIFU?
7. KWA NINI TUFURAHI?
8. KWA NINI TUSHIKE AMRI/
9. NINI MAANA YA KUHESABU.

   Baada ya kuona dondoo chache hapo juu, sasa naomba tufuatane pamoja katika maandiko/Neno la Mungu.

1Wathes. 5:16-18.
Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.


   Rafiki yangu mpenzi, na ijulikane kwako leo kuwa msingi wa furaha yetu katika Kristo Yesu ni ''Kumshukuru Mungu kwa kila jambo'' unalolipitia ( mstari 18 ) haijalishi linachoma kama moto. Hii ni amri ( mstari 16 ) na siyo hiari ndio maana anasema ndio mapenzi ya Mungu kwetu.
Kufurahi katikati ya dhoruba (storm) hakuji automatically bali ni pale mwana wa Mungu atakapotii na kufuata agizo/amri, FURAHINI SIKU ZOTE.

* Kufurahi ni AMRI.
* Kufurahi siku zote ni MBINU YA KIVITA.

Warumi 5:3-5
Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini.

Hapa Mungu anajaribu kutupa maana ya wazi kwa nini tufurahi hata pale ambapo kibinadamu inakuwa vigumu. Mara nyingi kabla Mungu hajamuinua mtu, hujaribu uvumilivu wake kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli kule jangwani. Mungu amefanya dhiki kuwa mtumishi wake mwaminifu ndio maana anasema ''DHIKI KAZI YAKE NI KULETA SABURI'' hivyo mtumishi dhiki amepewa kazi maalumu kwa utukufu wa Mungu Baba.

Saburi ni zaidi ya uvumilivu.
Kazi ya dhiki ni kuleta SABURI, Kazi ya saburi ni UTHABITI WA MOYO, na kazi ya uthabiti wa moyo ni TUMAINI.

* Saburi hujengeka tunapopitia katika dhiki.
* Dhiki ni mtumishi mwaminifu wa Mungu.
* Kufurahi sio suala la kujisikia bali ni KUAMUA.

Yakobo 1:2-4
Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno.

Oooh Asante Yesu kwa ajili ya rafiki yangu huyu ambaye anajifunza neno hili chini ya uvuli wa nguvu na uwepo wa ROHO MTAKATIFU.
Mungu anaposema, HESABUNI, anataka ufike mahali uelewe na utambue kuwa ''MUNGU YEHOVA amekuamini kuwa unaweza kuvuka kwa ushindi katika jaribu au jambo lolote unalolipitia sasa hivi au utakalolipitia.

Saburi ilikuwa na kazi njema katika maisha ya Yusufu, pamoja na uovu na mabaya mengi aliyotendewa hakumuacha Mungu, na mwisho wa saburi yake kulizaliwa TUMAINI ndani yake kwa ndugu zake na kwa taifa la Israeli kwa ujumla wake.
   Yusufu akawaambia, Msiogope, je! mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa , kama ilivyo leo. MWANZO 50:19-20
Tambua ya kuwa Mungu analo kusudi juu ya kila unalolipitia, ifike mahali ufunguke na kuwa na ujasiri wa kusema kuwa katika hili ninalolipitia uko mkono wa Bwana pamoja nami katika kunipatia mema. Paulo mtume alifika mahali akafunguka, akasema maneno mazito sana; ''KUISHI KWANGU NI KRISTO, KUFA NI FAIDA'', ''SI MIMI NIISHIE, BALI KRISTO NDANI YANGU'' Inahitaji ujasiri, ukomavu na kujitoa mzima mzima kwa BWANA.
Haya maisha tunayoishi leo sio yetu/sio yako, ni ya Mungu.

Mithali 19:16.
Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa.

   Watu wengi wanahesabu kuwa kuingia katika majaribu ni MKOSI, la hasha! Ni mapenzi ya Mungu kuwa AKILI zetu zifike mahali zitafsiri vema nyakati tunazokuwa tunazipitia. Unalitafsiri vipi hilo jaribu unalolipitia sasa hivi? Je unalitafsiri kuwa ni mkosi au kuwa Mungu amekuacha?
Tafsiri chanya ni kwamba, katika jaribu hili, SI MIMI NINAYEISHI BALI KRISTO NDANI YANGU; maana ameniamini kuwa naweza kuvuka, nami nitavuka tu. Zaidi sana nalihesabu jaribu hili kuwa ni fursa (opportunity) kulifikia KUSUDI, kupanda ngazi.

1Petro 4:12-14
Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. ... ; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.

   Rafiki yangu mpenzi, Neno la Mungu linatueleza wazi kabisa kuwa sio kitu kigeni au cha ajabu au mkosi tunapopita katika jaribu/nyakati ngumu.
Mtu mmoja alinena mahali fulani akasema hivi; NYAKATI NGUMU HAZIDUMU, BALI WATU WAGUMU (yaani walio thabiti wa imani) HUDUMU.
Zingatia hili: ILI NA KATIKA UFUNUO WA UTUKUFU WAKE MFURAHI KWA SHANGWE.

2Kor. 12:7-10.
Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu (jaribu) wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

Rafiki yangu mpenzi, Paulo mtume amemaliza kila kitu kwa kuweka bayana KUSUDI la mkristo kupitia nyakati ngumu, kusudi la Mungu ni ili kwamba yeye (MUNGU) atukuzwe. Ili uweza wa Mungu/Kristo udhihirishwe kwetu. Yaani uweza wa Kristo hutimilika ndani yetu kupitia udhaifu tulio nao au nyakati ngumu tunazokutana nazo ambazo kiukweli tusingeweza kuvuka bila yeye.

HITIMISHO.

* Furaha ni UFALME WA MUNGU - Warumi 14:17.
* Unapodumu katika furaha unakaa ndani ya Ufalme wa Mungu Yehova, unakaa katika uwepo wa Roho Mtakatifu.




















Salamu zangu mimi Mdee, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndio mwandiko wangu. Bwana na awe pamoja na roho yako.

DREAM BIG.

Contacts:

Mob.  0659 700 002
          0756 145 417
email: mdeebn@gmail.com








«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

1 comment:

Unknown said...

Barikiwa mtumishi kwa neno na ujumbe muafaka!


Juu