STORY FUPI INAYOWEZA KUBADILISHA MTAZAMO WA NDOA YAKO
“Nilipofika nyumbani usiku ule, mke wangu aliponitayarishia chakula, nilimshika mkono na kumwambia, Kuna kitu nataka nikwambie. Mke wangu alikaa chini na kula chakula kimya akiwa tayari kunisikiliza. Tena nikagundua macho yake yalionyesha anaumizwa. Nilishindwa hata namna ya kuanza kufumbua kinywa changu. Lakini ilibidi nimwambie ili ajue nilikuwa nikifikiri nini juu yake.
Nataka kukupa talaka. Nilianza kusema kwa utulivu. Alionekana kutokereka na maneno yangu badala yake aliniuliza kwa sauti ya upole ‘kwa nini?’ Sikumjibu swali lake. Kutojibu kulimfanya akasirike. Akatupa kijiko na akanikaripia, ‘wewe si mwanamume!’ Usiku ule, hakukuwa na maongezi kati yetu. Alikuwa akilia kwa kwikwi. Nilifahamu kwamba alitaka kujua ni nini kimetokea kwenye ndoa yetu. Lakini kwa hakika nisingeweza kumpa jibu wala sababu ya kuridhisha; alionekana si mali kitu kwangu penzi langu lilihamia kwa Judy. Sikumpenda tena mke wangu mawazo yote yalikuwa kwa Judy. Kwa kweli nilimdharau mke wangu!
Huku moyo wangu ukijua wazi kwamba nafanya kosa, niliandika talaka ambayo ilionyesha kwamba yeye (mke wangu) angepata nyumba yetu, gari na atakuwa na hisa 30% ya kampuni yetu. Aliangalia talaka ile na kuichana vipande vipande.
Mke ambaye tumeishi nami kwa miaka 10 alionekana mgeni machoni mwangu. Nilimuonea huruma kwa muda, rasilimali na nguvu alizopoteza lakini sikuweza kurudi nyuma kwa sababu Judy aliuteka moyo wangu kisawasawa. Hatimaye mke wangu alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo kwa hakika nilitarajia. Kwangu mimi kilio chake kilinipa nafuu.
Wazo la kuachana na mke wangu limenisumbua kwa majuma kadhaa na sasa limeendelea kuimarika na kuwa jambo la hakika zaidi.
Siku iliyofuata nilikuja nyumbani kwa kuchelewa sana nikakuta mke wangu akiandika jambo mezani. Sikutamani hata kula chakula alichonipikia nilikwenda moja kwa moja chumbani na usingizi ulinichukua mara moja kwa sababu nilikuwa nimechoka baada ya kula raha za kufa mtu na Judy.
Usiku nilishtuka usingizini mke wangu alikuwa bado akiandika. Sikujali kabisa nikajifunika vyema shuka na kulala tena. Asubuhi yake alinikabidhi masharti ya talaka yake: hakutaka kitu chochote kutoka kwangu lakini alihitaji apate angalau mwezi mmoja wa kujiandaa kabla hajaachika. Akaomba kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja sote mimi na yeye tujitahidi kuishi maisha ya upendo au kawaida kwa kadiri itakavyowezekana. Sababu yake ilikuwa ndogo lakini muhimu: mwanetu wa kiume alikuwa akikaribia kufanya mtihani katika mwezi uliofuata kwa hiyo hakupenda mtoto aathirike kisaikolojia kwa sababu ya kuachana kwetu. Hili halikuwa tatizo kwangu, nilikubali mpango wake. Lakini alikuwa na sharti la ziada, aliniomba nikumbuke jinsi nilivyombeba siku za fungate yetu hasa siku ya harusi yetu. Akaniomba na kunisihi kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja niwe nambeba kutoka kitandani kwetu mpaka mlango wa kutokea kila asubuhi. Nilidhani anakaribia kuwa kichaa. Ili kufanya siku zetu za mwisho zisiwe na migogoro nilikubaliana na masharti yake ya ajabu.
Nilimsimulia Judy kuhusu masharti ya kuachana na mke wangu. Judy alicheka sana, aliona ni ujinga. ‘Hata akitumia ujanja wa namna gani talaka ni lazima’, alisema Judy tena kwa dharau. Mimi na mke wangu hatukuwahi kugusana tangu nilipomweleza dhamira ya kumtaliki. Kwa hiyo nilipombeba kwa mara ya kwanza sote tulinuniana. Mwanetu alifurahi sana na kupiga makofi nyuma yetu, ‘aah baba kambeba mama mikononi mwake’. Maneno yake yalinichoma moyoni moja kwa moja. Kutoka chumbani kwetu hadi sebuleni, halafu tena mpaka mlangoni, ni zaidi ya mita kumi nimembeba mke wangu. Alifumba macho na kusema kwa sauti laini na ya upole; usimwambie mwanetu juu ya talaka. Nilikubali kwa kichwa, ingawa nilijisikia vibaya. Nilimuweka chini nje ya nyumba.
Alienda kituoni kusubiri basi la kazini kwake nami nikaendesha gari kwenda ofisini kwangu. Siku ya pili, zoezi lilikuwa rahisi kwetu sote. Aliegemea kifuani pangu. Nilisikia harufu nzuri ya uturi aliofukiza kwenye blauzi yake. Nikagundua kwamba sijamuangalia kwa makini mke wangu kwa kipindi kirefu sana. Nikagundua hakuwa binti tena. Kulikuwa na mikunjo usoni na nywele zake zilianza kuwa nyeupe! Ndoa yetu imekula urembo wake. Kwa dakika moja nikafikiri kwa nini namfanyia hivi.
Siku ya nne nilipombeba hisia za mapenzi kati yetu zilirejea. Huyu ni mwanamke aliyejitoa kuishi nami na tumeishi kwa miaka kumi sasa. Siku ya tano na ya sita ilikuwa wazi kwamba mapenzi yetu yalikuwa yakimea upya. Sikumwambia Judy kuhusu jambo hili. Kadiri mwezi ulivyokaribia kwisha niliona raha kumbeba mke wangu na zoezi likawa rahisi zaidi. Pengine kufanya kazi hii kila siku kuliniimarisha zaidi.
Alikuwa akichagua nini cha kuvaa asubuhi. Alichagua mavazi kadhaa hakupata linalomfaa. Kisha akaguna, ‘nguo zangu zote zimekuwa kubwa’. Nikagundua kwamba mke wangu amepungua sana, nadhani ndiyo maana niliweza kumbeba kirahisi. Ghafla jambo likanichoma... mke wangu ana uchungu na maumivu makuu moyoni mwake. Bila kujitambua nikamgusa kichwa chake. Mara mtoto wetu akatokeza na kusema ‘baba ni wakati wa kumbeba mama muende kazini’. Kwake kumuona baba akimbeba mama likawa ni jambo la furaha sana. Mke wangu alimuonyesha ishara mwanetu asogee karibu na akamkumbatia kwa upendo mkuu. Niligeuza uso wangu nisije nikabadili mawazo katika dakika ya mwisho. Kisha nikambeba mikononi mwangu kutoka chumbani, sebuleni halafu mpaka mlangoni. Mkono wake laini ulikuwa umeizunguka shingo yangu kwa upendo. Nilimkumbatia mwili wake; ilikuwa ni mithili ya siku ya ndoa yetu. Lakini wepesi wake ulinitia mashaka.
Siku ya mwisho nilipombeba nilipata shida hata kupiga hatua moja. Mtoto wetu alishakwenda shuleni. Nilimshika kwa karibu na kumwambia sikubaini kwamba maisha yetu yalikosa upendo. Nikaenda zangu ofisini…. Nikashuka garini hata bila kufunga mlango. Maana nilihisi nikichelewa tu ninaweza kubadili nilichoamua.... nikapanda ngazi. Judy alifungua mlango nikamwambia, ‘Samahani, Judy, sihitaji tena kumtaliki mke wangu’. Akaniangalia kwa kustaajabu, halafu akagusa kichwa changu. Akaniuliza ‘Unaumwa?’ Nikaondoa mkono wake kichwani kwangu. ‘Samahani, Judy, nimesema sitaki kumtaliki mke wangu. Nadhani ndoa yangu haikuwa na furaha kwa sababu sikuthamini undani wa maisha yetu, mimi na mke wangu, si kwamba hatupendani. Nimetambua hilo tangu nilipombeba siku ya ndoa yetu nilitakiwa kumbeba siku zote za maisha yetu, nampenda mke wangu sitamuacha mpaka kifo kitakapotutenganisha.’
Ikawa kama Judy alizinduka usingizini. Akanizaba kibao cha nguvu, akajiegemeza mlangoni na kuanza kulia. Nikashuka ngazi na kuondoka zangu. Nikaingia kwenye duka la maua nikaagiza maua mengi mazuri kwa ajili ya mke wangu. Muuzaji akaniuliza aandike nini kwenye kadi. Nikatabasamu na kuandika “Nitakubeba kila asubuhi mke wangu mpaka kifo kitakapotutenganisha”. Jioni ile nilifika nyumbani na maua mikononi mwangu, tabasamu kubwa usoni nikakimbia mpaka chumbani, nikapokelewa na maiti ya mke wangu kitandani.
Kumbe mke wangu alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa miezi kadhaa nami nilishindwa kubaini kwa sababu nilihamishia akili yangu kwa Mary. Alijua kwamba angekufa karibuni na alitaka asiniingize katika chuki na mwanetu kama ningelazimisha talaka mapema.
Angalau machoni mwa mwanangu naonekana ni mume mwema.
Ni Wewe_Ebenezer praise team!
Bonyeza kitufe cha play kusikiliza wimbo huu.
Toa maoni yako, story hii imekusaidia?
Source: Mary Muna.
KUMBUKA:
Kama ambavyo Blog hii imekuwa ikikuletea mafundisho yenye kubadilisha ufahamu/akili na maisha kwa ujumla; Unaweza kui-support Blog hii kwa kununua mafuta halisi ya alizeti yenyo ubora wa juu, Lengo ni kufanikisha Blog hii Iendelee kukuletea mafundisho mazuri kutoka kwa watu maarufu na waliofanikiwa ambao nimekuwa nao bega kwa bega ili kuhakikisha msomaji wangu anapata kitu kitakachoweza kumtoa hatua moja kwenda hatua nyingine!
Ili kujipatia Mafuta haya waweza kuwasiliana nasi kwa 0659 700 002 na Mungu atakubariki.
Asanteni sana wadau wangu!
No comments:
Post a Comment