Yatupasa wote tuliopo katika mahusiano, kabla ya kuendelea na kufanya maamuzi fulani tuwe tunatazama pia dalili za hatari. Kwa upande mkubwa dalili hizi zimeegemea kuwasaidia zaidi jinsia ya kike kujua au kuwafahamu wanaume. Hii ni kwa sababu wanawake ndio ambao wamekuwa wakioyesha kuumizwa zaidi na kukatishwa tamaa na mabadiliko ya tabia za wanaume mara wanapozama katika dimbwi la mapenzi. Ingawa wapo pia wanaume wanaoumizwa kutokana na mabadiliko ya tabia za wapenzi wao, na wao pia waweze kuzitazama dalili hizi.
DALILI ZENYEWE HIZI HAPA:
1. Mpenzi wako anakuwa na wivu sana kwa ule muda unaotumia kuwa na wafanyakazi wenzako,
marafiki na hata ndugu zako, ingawa sio kwamba anataka muda huo awe na wewe.
2. Anakuwa na tabia za kukuudhi na kukutawala, ataangalia sana kutoka na kuingia kwako, nyendo zako
na hata matumizi yako ya fedha, na kama ukimuuliza kwanini anafanya hivyo atajitetea kuwa anakusaidia
kufanya maamuzi sahihi.
3. Taratibu anakutenga na wote waliokaribu na wewe, pia anajaribu kukutenga na wale wanaoonekana
kuwa msaada kwako kama vile wale unaowasiliana nao kwa simu, wafanyakazi wenzako na hata ndugu
zako wa karibu.
4. Huwa na tabia ya kuwalaumu sana wengine kwa matatizo anayoyapata yeye. Mfano anapokosa kazi,
anaposhindwa shuleni, anapokosa pesa nk. Kila kitu ni kosa la mtu mwingine na sio yeye.
5. Hukasirishwa na kuudhiwa na vitu vidogo vidogo na vya kawaida katika maisha ya kila siku, mfano
akiambiwa afanye kazi zaidi ya muda wa ofisi, akiombwa amwangalie mtoto, anapopingwa katika kitu
kidogo nk.
6. Anakuwa na tabia za kikatili kwa wanyama wafugwao “pets” na hata kwa watoto. Haumizwi pale
anapoona maumivu au kuteseka kwa kiumbe kingine. Anaweza kujiona anacheza au anatania bila kujua
anamuumiza mtoto au mnyama.
7. Ni wenye tabia ya mabavu hususan katika tendo la ndoa, hawatojali hisia zako, umelala usingizini au
unaumwa, bali hujali zaidi kuzitimiza haja zao.
8. Ni wenye maneno makali yakuumiza na ya kushusha hadhi, huweza kukuamsha usingizini ili akutukane au
kukugombeza. Akianza malumbano hakupi upenyo wa kwenda kulala, anaweza kulalama usiku mzima.
9. Sio watu wakutabirika, ni watu wenye hisia za kubadilika badilika, mara muda huu anafuraha na
kuonyesha mapenzi, mara ghafla kakasirika na kutaka kuadhibu mtu.
10. Anaweza akawa na historia ya tabia za kikorofi na kigomvi, labda amewahi kuwa na matukio ya
kuwapiga marafiki zake, akijitetea kuwa alipitiwa tu na hasira.
11. Ni mwenye vitisho na tabia za kuashiria fujo, mfano kupenda kutishia akisema “nitakuzaba vibao”
“nitakuuwa ‘I will kill you if….”, “nitakuvunja shingo”, “nitakufanyia kitu mbaya” n.k.
12. Mwenye tabia ya kupiga au kugonga vitu kwa hasira, kuvunja vitu vyako, kukurushia vitu wewe au
watoto kwa hasira.
13. Hutumia nguvu anaposisitiza hoja yake, mfano, kukushika nguo au kukukandamiza ukutani na mara
nyingine kukusukuma.
• Tafiti zimegundua kwamba, kama mtu anaonyesha tabia za fujo na kijeuri wakati wa urafiki au uchumba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa mtu wa hatari zaidi mara atakapoingia kwenye ndoa. Kamwe usijidanganye na kujifariji kwamba hivyo vijitabia anavyovionyesha sasa eti atabadilika tu mara mkioana. Sahau.
Kumbuka; fujo huzaa fujo, na ujeuri huzaa ugomvi na kwa haraka vyote hivi huua mapenzi kwa wale wanaopendana.
CHRIS MAUKI - Mtaalamu wa Saikolojia Ya Jamii na Ushauri.
KUMBUKA:
Kama Blog hii imekuwa ya baraka kwako, unaweza kui-support kwa kununua bidhaa yetu ya Mafuta Halisi Ya Alizeti ili kuendelea kukuletea mafundisho zaidi kutoka kwa watu mbalimbali waliofanikiwa.
Bei zetu ni nzuri na mafuta haya yanapatikana kwa bei za Jumla na Rejareja!
Wasiliana nasi kwa:
0659 700 002. Asanteni na Mungu awabariki wadau wangu!
No comments:
Post a Comment